Home Habari za michezo INJINIA HERSI AANZA KWA KISHINDO URAIS YANGA…MFUMO WA MATAWI KUTUMIKA KUIUNGANISHA KLABU…

INJINIA HERSI AANZA KWA KISHINDO URAIS YANGA…MFUMO WA MATAWI KUTUMIKA KUIUNGANISHA KLABU…


Rais  wa klabu ya Yanga, Hersi Said amesema baada ya kumaliza Uchaguzi Mkuu wanaenda kurudisha umoja na kutekeleza vipaumbele walivyoahidi huku akiomba ushirikiano kutoka kwa viongozi wa matawi.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa zoezi la Uchaguzi Mkuu juzi alisema wanahitaji kujenga umoja wao ili kwenda kupigana na adui nje na kuwashukuru wanachama wote walioshiriki kupiga kura, wajumbe waliogombea na viongozi waliopita.

“Niwashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kutoka mikoa mbalimbali kwa kutumia gharama zenu wenyewe na kuja kushiriki uchaguzi, sasa tumefunga uchaguzi Yanga inarudi kuwa moja,”alisema.

Alisema katika uongozi wake atahakikisha anasimamia mahusiano yote waliyoahidi kwa wanachama hao na kuomba matawi kuendelea kushirikiana kuipeleka Yanga mbele kama ilivyokusudiwa. Hersi alimshukuru Mwenyekiti mstaafu wa Yanga, Dk Mshindo Msolla na kamati yake akisema kwake yeye kiongozi huyo ni mhimili kupata ushauri wake huku akiahidi kumrejesha mgombea nafasi ya Makamu wa Rais aliyeshindwa Suma Mwaitenda kufanya naye kazi.

Alisema ana nafasi mbili kikatiba kuchagua wajumbe wawili wa kuongeza kwenye Kamati ya Utendaji. Mwaitenda alishindwa na Arafat kwa kura 545 huku yeye akipata kura 234 kwa wapiga kura 785 na kura sita zikijaribika. Wajumbe watano walioshinda kati ya 17 walioshiriki ni Yanga Makaga aliyepata kura 519, Munir Seleman kura 330, Alexander Ngai kura 327, Rodgers Gumbo kura 376 na Seif Gulamali kura 478.

Washindi wote watafanya kazi na Rais Hersi kuhakikisha Yanga inapata miundombinu bora ya uwanja, kuendelea kushinda makombe, kuimarisha uchumi imara ndani ya klabu, uwekezaji soka la vijana, wanawake na kuendeleza ushirikiano wao na matawi, wadau na serikali.

SOMA NA HII  BENCHI LAMFANYA MPOLE KUTEMBEA NA MKATABA WA SIMBA KWENYE BEGI....AFUNGUKA HAYA KUHUSU HATMA YAKE....