Home Habari za michezo KUELEKEA MSIMU UJAO…DENIS NKANE AANZA ‘KUPULIZA MOTO’ YANGA…AZITISHIA ‘NYAU’ SIMBA NA AZAM...

KUELEKEA MSIMU UJAO…DENIS NKANE AANZA ‘KUPULIZA MOTO’ YANGA…AZITISHIA ‘NYAU’ SIMBA NA AZAM FC…


WINGA wa Yanga Denis Nkane amesema yeye na wachezaji wenzake wa timu hiyo wameambizana kuhakikisha wanachukua vikombe vyote kwa mara nyingine na si vitatu tena, bali hata vile ambavyo vitakavyoongezeka.

Maneno hayo ya ujasiri ni kama kuzitisha klabu za Simba na Yanga ambazo nazo msimu huu zimesajili wachezaji mahiri kwa malengo ya kutwaa mataji, ikiwemo Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza akiwa kambini Kigamboni ambako kikosi cha Yanga kimeweka kambi, Nkane ambaye kwa sasa wachezaji wenzake wamemtungia jina jipya la utani ‘Boy From Buza’, amesema wao kama wachezaji wanaendelea vizuri na mazoezi ya fizikia na kuuchezea mpira, lengo ni kufanya vema msimu ujao kuwafurahisha wanachama na mashabiki wa Yanga

“Kambi inakwenda vizuri, tunafanya mazoezi yote ya kuweka mwili sawa na kuuchezea mpira. Msimu ujao naamini kama mchezaji nina deni kubwa kwenye michuano ya ndani na nje ya nchi.

Naamini hili litafanyika nikiwa na ushirikiano na wachezaji wenzangu, tumejipanga kuchukua tena mataji yote matatu, ni kitu kinachowezekana kabisa na kama vingine vitaongezeka navyo tutavichukua,” alisema Nkane, mchezaji aliyesajiliwa kipindi cha dirisha dogo msimu uliopita, akitokea Biashara United ambayo msimu ulipomalizika ikashuka daraja.

Alisema kuwa amejifunza vitu kadhaa kutoka kwa wachezaji Stephane Aziz Ki na Gael Bigirimana, kwa sababu ni wachezaji wakubwa na wameshacheza michuano mbalimbali mikubwa kuliko yeye.

“Nimefurahi na najivunia kucheza nao kwa sababu ni wachezaji wakubwa na mimi najifunza vitu kadhaa kutoka kwao, naamini muda utaongea na wanachama na mashabiki wa Yanga watafurahi,” alisema.

Kikosi cha Yanga kinaendelea na mazoezi, huku wachezaji wawili wakiwa bado hawajawasili, nao ni Yannick Bangala na Bernard Morrison aliyesajiliwa kutoka Simba.

Licha ya kujiandaa na msimu mpya wa mashindano, lakini Yanga kwa sasa inajiandaa na tamasha la Wiki ya Mwananchi, kilele chake kikitarajiwa kufanyika Agosti 6 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, itakapocheza mechi, huku taarifa za ndani zikidai kuwa huenda ikacheza dhidi ya Vipers FC ambao ni Mabingwa wa Uganda.

SOMA NA HII  YANGA WATUA NIGERIA,MATIZI KUPIGA LEO