Home Habari za michezo KUFUZU CHAN…STARS KUMALIZIA KAZI YA ‘KUSAFISHA JALALA LEO’…WAKIZINGUA NDIO BASI TENA…

KUFUZU CHAN…STARS KUMALIZIA KAZI YA ‘KUSAFISHA JALALA LEO’…WAKIZINGUA NDIO BASI TENA…


HATMA ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kwenda kwenye hatua inayofuata kwa ajili ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani (CHAN), itafahamika leo itakaporudiana na Somalia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Stars inaingia uwanjani ikiwa na mtaji wa bao moja ililolipata Jumamosi iliyopita kwenye uwanja huo huo, ilipoinyuka timu ya taifa ya Somalia bao 1-0 lililofungwa na Abdul Selemani “Sopu’ dakika moja baada ya mapumziko.

Wakati Stars ikihitaji ushindi au sare ya aina yoyote ili kuweza kusonga mbele, wageni Somalia wanahitaji ushindi wa zaidi ya bao moja ili kuweza kupita kwenye raundi inayofuata.

Timu yoyote itakayosonga mbele itakutaka na timu ya taifa ya Uganda, The Uganda Cranes.

Jumamosi iliyopita, timu hizo zilicheza kwenye uwanja huo huo, lakini kikanuni Somalia ilihesabika kuwa ipo nyumbani, baada ya wao wenyewe kuomba hivyo, kutokana na usalama mdogo kwenye nchi yao.

Kocha Mkuu wa timu hiyo Kim Poulsen amesema kuwa anatumaini mchezo wa leo utakuwa mzuri, tofauti na mechi iliyopita huku akiweka wazi kuwa watamkosa golikipa, Aishi Manula.

“Wachezaji wote wako sawa, isipokuwa Aishi ambaye aliumia kwenye mechi iliyopita, tumejiandaa kucheza kwa kushambulia zaidi na hapo hapo kujilinda ili tusiruhusu bao, falsafa yetu ni kupigiana pasi zaidi na kushambulia,” alisema kocha huyo.

Aidha Poulsen alisema wachezaji wake wapo tayari kwa mchezo huo na anauchukulia kwa umuhimu mkubwa.

Kwa upande wake Aishi Manula alisema wachezaji wamejipanga kupata matokeo mazuri tofauti na waliyoyapata kwenye mchezo uliopita.

“Tumejipanga kupata matokeo bora katika mchezo huo tumeshawasoma wapinzani wetu tunaomba watanzania waendelee kutuombea na kutupa sapoti,” alisema Manula.

“Mechi iliyopita tulikuwa na matarajio makubwa, lakini haikuwa kama tulivyotarajia, lakini kwenye mechi hii tuna uhakika kwa sababu tayari tumeshawaona jinsi wanavyocheza, jinsi walivyoweza kujilinda vizuri na sisi leo kama alivyosema mwalimu, tunakwenda kushambulia zaidi,” alisema.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUDAKA MECHI ZOTE KWA KIWANGO KIKUBWA...HAULE AIBUKA NA HILI KUHUSU MSHERY...AMTAJA DIARRA...