Home Habari za michezo SIKU CHACHE BAADA YA KUJIUNGA SIMBA…KAPAMA AIBUKA NA KUANIKA MAUZAUZA ALIYOWAHIKUTANA NAYO...

SIKU CHACHE BAADA YA KUJIUNGA SIMBA…KAPAMA AIBUKA NA KUANIKA MAUZAUZA ALIYOWAHIKUTANA NAYO …


Ndani ya Simba kuna mabeki wa kati Henock Inonga, Joash Onyango na Kennedy Juma baada ya kuachana na Pascal Wawa ambaye hawajamuongezea mkataba mpya baada ya ule wa awali kumalizika.

Lakini sasa kuna kirak  a kutoka Kagera Sugar, Nassoro Kapama ambaye amepewa mkataba wa miaka miwili akimudu kucheza beki ya kati, kiungo mkabaji na pia mshambuliaji. Hivi karibuni nyota huyo alifanya mahojiano maalumu na kuelezea mambo mbalimbali juu ya soka lake.

“Nacheza nafasi nyingi, ila namuachia kocha ni nafasi gani atanitumia, lakini kwa upande wangu kwa Simba ilivyo sasa naiona nafasi beki wa kati naamini nikiaminiwa na kupewa nafasi nitafanya makubwa au kiungo mkabaji pia naweza kucheza,” anasema.

BAO LA KICHWA

Akizungumzia matukio aliyokutana nayo katika soka, Kapama anasema: “Nimecheza soka kwa muda mrefu, nimekutana na matukio mengi kama kuchinja paka, kumfukia paka makaburini, kufukua makaburi na kulala makaburini kwa baadhi ya wana kamati wa timu lakini kuna tukio sitakaa nikalisahau.

“Nimewahi kucheza mechi ya ndondo ambayo ilikuwa ni fainali ilitukutanisha sisi na timu yangu ya mtaani, tulicheza na wahuni wa Keko kwenye Uwanja wa Keko JK. Ile mechi ilichezwa nusu uwanja kwa sababu wahuni wa Keko upande wa lango lao walikuwa na mashabiki wao wahuni, wengi ukisogea tu chupa zinakuhusu hivyo tulikuwa tunapiga mashuti ya mbali.” Kapama anasema mpira uliisha kwa wao kushinda bao moja, lakini haikuwa rahisi hadi gari ya polisi ilipofika uwanjani hapo na mpira kuchezwa uwanja mzima. “Nakumbuka nilikuwa na kina Idd Nado na Hassan Dilunga,” anasema.

“Tukio lingine ambalo sitakaa nikasahau kwenye maisha yangu ni siku ambayo tulikuwa tunacheza mechi mtaani kwetu, kwenye uwanja wa mtaani kwetu Mbagala Rangi tatu mtaa wa Kiburugwa, nilifunga bao la kichwa bahati mbaya nilichanganyikiwa hapo hapo mara tu baada ya kufunga.

“Baada ya bao nilijikuta nipo nje ya uwanja na kuwaaga wenzangu kuwa naondoka. Walihoji kwanini? Jibu lilikuwa siwezi kuendelea kucheza nataka kuondoka, nilipofika sikumbuki nilifika vipi nyumbani zaidi nilishtuka saa kumi kumi alfajiri ndio akili yangu imekaa sawa na najitambua.”

KISA NDEGE AKOSA USINGIZI

Kapama ana stori nyingi za kusisimua za matukio aliyowahi kupitia ikiwemo kukosa usingizi siku ya kwanza kupanda ndege. “Hadi sasa nilipofikia nimewahi kupanda ndege mara moja tu. Nakumbuka siku nilipoambiwa natakiwa kupanda nilikosa usingizi kabisa na sikuwa na amani moyoni kutokana na woga na tukio hilo kutokea kama ndoto kwangu,”anasema

“Siku ya kwanza kupanda ndege ni siku tulipoipandisha Ndanda FC 2014 (Ligi Kuu) tulitoka na ndege kutoka Dar es Salaam hadi Mtwara. Kiukweli sikuwa na amani kama wengine waliofurahia tukio hilo.

“Usafiri wa maji na gari kwangu hauna shida kabisa, lakini suala la ndege itabidi niwe na njia mbadala kama kumeza dawa au kuchomwa sindano ili kupunguza presha.”

AMTAJA LUIS SIMBA

Kapama ambaye alikotoka alikuwa anavaa jezi namba 11 inayovaliwa na Peter Banda kwa sasa, ameibuka na kuikana namba hiyo ambayo amekiri kuchaguliwa na mama’ke mzazi kwa kuweka wazi kuwa atavaa namba yoyote atakayopewa.

“Nakumbuka nilivyokuwa natua Kagera Sugar nilimpigia mama simu na kumuuliza nivae jezi namba ngapi? Aliniambia 11, sikuhoji sababu, nikaamua kuivaa lakini kwa sasa baada ya kutua Simba siitaki.

“Naogopa kuivaa jezi hiyo kwa sababu imevaliwa na staa mkubwa ambaye ni Luis Miquissone amefanya mambo makubwa ndani ya Simba ambayo wana Simba wanatamani kumuona tena, hivyo nahitaji na mimi kuvaa jezi yangu ambayo itanijengea ufalme,” anasema Kapama na kwamba kucheza Simba au Yanga ilikuwa moja ya ndoto zake

MATUMAINI KIBAO KIMATAIFA

Nyota huyo ana matumaini kwamba watafanya vizuri kimataifa msimu ujao, akisema‚ “nimefika Simba wakati muafaka kipindi ambacho wamepata nafasi ya kuiwakilisha nchi kimataifa. Nina matumanini makubwa ya kutumia nafasi niliyoipata kufanya kile nilichonacho mguuni kwangu kwa kuhakikisha nakuwa mmoja wa wachezaji wanaofikia malengo ya klabu.

“Mbali na kuipambania Simba ni nafasi yangu kujitangaza kimataifa. Ndoto yangu ya kwanza imetia kwa kucheza timu ya ndoto yangu, bado nina safari ndefu kufikia malengo yangu ya kutoka Simba na kucheza kimataifa. Nitatumia mashindano haya kujiweka sokoni kwa kufanya vizuri zaidi.”

SOMA NA HII  UCHAGUZI MKUU SIMBA:..MWANACHAMA 1000 TU KUPIGA KURA LEO...MAMBO YA KUZINGATIA HAYA HAPA...

SH1.5 mil YAKATISHA NDOTO ZAKE

Kapama anasema: “Ndoto yangu mbali na soka nilikuwa natamani kufuata nyayo za baba yangu yangu ambaye ni mwanajeshi, alishawahi kukaa na sisi wanawe na kutuambia anatamani mwanawe mmoja afuate nyayo zake mipango ilikuwa mimi. “Baadaye ndoto za kuwa mjeshi zilikata nikiwa na Ndanda FC. Nakumbuka baada ya kuipandisha daraja msimu wa 2014 nilipata Sh1.5 milioni nikaona maisha ya mpira ndio kila kitu na kuamua kuanza maisha ya kujitegemea kwa kununua mahitaji.”

PRESHA ITAMKOMAZA

Mchezaji huyo anaamini kucheza kwa presha kutamfanya akomae zaidi. “Nafahamu kuwa matarajio ya mashabiki wa Simba ni makubwa kwangu, wanatamani kuona nafanya mambo makubwa zaidi ya niliyoyafanya nikiwa Kagera Sugar, nimejiandaa kufanya hivyo.

“Simba ina presha kubwa kutokana na wingi wa mashabiki tofauti na nilikotoka nitatumia ushabiki wao kufanya mambo makubwa, mabaya yao kwangu nitayachukulia kama changamoto mazuri yao kwangu yataongeza nguvu kwangu kupambana zaidi.”

SURE BOY, MKUDE HABARI NYINGINE

Akiwazungumzia nyota wazawa wanaocheza kama viungo, Kapama anasema: “Nimekutana na viungo wengi wazuri ndani ya misimu niliyocheza ligi, wachezaji ambao kwangu ilikuwa ni mtihani nikikutana na timu zao – ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Jonas Mkude. Siku tukiwa na mechi na timu wanazochezea nilikuwa najiandaa vya kutosha. Ni wachezaji wazuri hasa wakiwa na mpira kuwakaba inahitaji kutumia akili na sio nguvu, ukicheza nao kwa nguvu lazima uonyeshwe kadi ni kutokana na namna wanavyocheza. Kwa upande wangu ndio zao bora la viungo kwa wazawa japo tumeongezeka kuwa wengi eneo hili.”

TIMU SITA, NYEKUNDU MOJA TU

Licha ya kucheza timu sita katika maeneo tofauti, lakini Kapama ana kadi moja tu yekundu. “Mwamuzi Heri Sasii, ndiye aliyewahi kunionyesha kadi nyekundu na iliniumiza sana kwani sina hakika kama lile tukio lilistahili kadi, siku zote naamini alinionea,” anasema. “Nakumbuka nikiwa Ndanda mechi ya kuamua sisi kupanda Ligi Kuu tulikuwa tunaongoza bao 1-0 dakika zilikuwa zimebaki kidogo mpira ulitoka ukawa ni wa kurusha upande wetu na mimi ndiye niliyekuwa karibu na mpira nikauokota na kumsubiri mrushaji kwa upande wetu. “Sasii alinisisitiza nirushe mimi nisiporusha nikiweka chini au kumpa mtu mwingine atanionyesha kadi nyekundu na mimi sikurusha kweli niliweka chini ili arushe anayepashwa kurusha na ndipo nilipopewa nyekundu.”

BANGALA ANASTAHILI

Yanick Bangala ni kiraka wa Yanga ambaye ameibuka mchezaji bora msimu huu tuzo za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Kapama anasema wamefanya chaguo sahihi.

“Naungana na TFF kumpa tuzo Bangala ni mchezaji ambaye kwa upande wangu ameniongezea vitu kutokana na kumfuatilia na kujifunza kitu kutoka kwake. Amekuwa bora kila eneo alilopewa nafasi ya kucheza,” anasema na kwamba chipukizi Dickson Mhilu naye alistahili kupewa tuzo hiyo.

“Mhilu amepata ofa nyingi baada ya ligi kumalizika, mimi kama kaka yake amenishirikisha nimekuwa mshauri wa kwanza kumwambia aendelee kubaki Kagera Sugar kwa misimu miwili zaidi ili akomaze akili, namshukuru amenielewa.”

SOKA LIMEMLIPA

Nyota huyo kacheza soka na limemlipa vizuri. “Kwa namna moja au nyingine naweza kusema soka limenilipa na nalidai kwa sababu limenipa nyumba ya kuishi. Pia nimeweza kumjengea mama yangu nyumba na natembelea gari. Mali zote zimetokana na kazi yangu ya soka si haba. “Pamoja na yote hayo bado sijafikia malengo yangu ambayo nimejiwekea maalumu kutokana na kazi yangu ya soka ambayo muda wa kustaafu ukifika mipango ni kuwa mfanyabiashara mkubwa,” anasema Kapama anayefurahia zaidi kucheza namba sita (kiungo mkabaji).

KIKOSI BORA

Anataja kikosi chake bora kuwa ni Abutwalib Mshery, Dickson Mhilu, Charles Luhende, Yanick Bangala, Abdallah Mfuko, Nasoro Kapama, Kichuya, Abdallah Seseme, Fiston Mayele, Feisal Salum na Yahya Zaydi.