Home Habari za michezo TFF NAO WAHUKUMIWA…BASI LA TAIFA STARS KUPIGWA MNADA HADHARANI KULIPA MADENI….

TFF NAO WAHUKUMIWA…BASI LA TAIFA STARS KUPIGWA MNADA HADHARANI KULIPA MADENI….


Baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuliamuru Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kulipa deni la Sh 56,446,700, wakili wa Taasisi za Filbert Bayi, Karoli Tarimo amefungua maombi kukazia hukumu akiiomba mahakama iruhusu kulikamata basi la TFF lenye namba za usajili T581 CGR liuzwe ili kulipa deni hilo.

Taasisi hiyo inaidai TFF fedha hizo kwa miaka mitatu ambazo kwa mujibu wa Tarimo zilikuwa ni gharama ya kambi kwa timu za vijana chini ya miaka 13, 15, 17 na ile ya wanawake katika taasisi hiyo Kibaha mkoani Pwani.

Alisema Juni 3, 2019 taasisi hiyo iliingia makubalino na TFF ya miaka mitatu kutoa huduma za viwanja, usafiri, kambi na chakula wenye thamani ya Sh521.4 milioni ambazo walikubaliana zilipwe kwa awamu na kusalia Sh76.4 milioni ambazo Julai 20, mwaka jana rais wa TFF, Wallace Karia alikiri katika mahojiano na  na kusema suala hilo lilikuwa linashughulikiwa.

Hata hivyo, Tarimo alisema baada ya TFF kutoonyesha dalili za kulipa ndani ya makubalino walifungua kesi Mahakama ya Kisutu na TFF ilikubali kudaiwa na kuahidi kulipa kwa awamu kuanzia Novemba, 2021 hadi Aprili 2022. Hata hivyo tangu ilipe awamu mbili haijalipa tena.

“Mei 17 tulifaili maombi kukazia hukumu kuomba kukamatwa gari la TFF na kuliuza. Maombi yamesikilizwa Julai 21 na shauri limeahirishwa hadi Agosti 4,” alisema.

Ofisa wa Sheria TFF, Herman Kidifu alipoulizwa alisema hana taarifa na kuomba aulizwe mwenyekiti wa kamati ya mashindano, Boniface Wambura ambaye simu yake iliita bila kupokewa jana.

SOMA NA HII  NDEMLA AZIDI KUJICHIMBIA MIKOANI....SINGIDA BIG STARS WAMCHOTA JUU KWA JUU KWA DAU NONO...ASALIMU AMRI...