KAMBI ya Simba imezidi kunoga kwa kocha Zoran Maki akiendelea kuwapika vijana wake, huku akimkomalia John Bocco, lakini nyota mpya wa timu hiyo Nelson Okwa amevunja ukimya na kuamsha vita ya namba kikosini akitamba kwamba yeye nafasi yoyote atakayopangwa ataliamsha.
Okwa aliyesajiliwa na Simba kutoka Rivers United na akitarajiwa kutambulishwa leo Jumatatu ikiwa ni siku chache kabla ya kambi ya timu hiyo iliyopo jijini Ismailia, Misri kuvunjwa, huku akisema amekiangalia kikosi na kubaini kina watu kwelikweli, lakini bado haimpi presha kwa vile anaamini kipaji chake na akipangwa kokote analiamsha.
Kiungo mshambuliaji huyo alisema huwa anafurahi kucheza kama mshambuliaji namba 10 au winga wa kushoto ambayo ndani ya Simba ina watu wa maana akiwamo Clatous Chama, Pape Ousmane Sakho na Moses Phiri, lakini bado anaamini atapenya kikosini.
“Nimekiangalia kikosi, kina watu wa maana kwelikweli. Nafurahia kutua timu kama hii na naamini itafika mbali michuano ya ndani na kimataifa, ila kazi itakuwa kwa kocha (Zoran) kuamua wapi pa kunipanga. Nafurahia sana kucheza kama mshambuliaji wa pili au winga wa kushoto,” alisema.
Mshambuliaji huyo alisema Simba imemsajili kwa kuamini kuwa ana kitu cha ziada cha kuisaidia timu na hilo ndilo jukumu la kwanza atakalofanya kwa kuipigania iwe katika Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika ambako anajua wanachama na mashabiki wana kiu ya kuona inafika mbali zaidi.
Wakati Okwa akiyasema hayo, Kocha Zoran ameendelea kugawa dozi kwa wachezaji, huku akimkomalia Bocco, akimtaka kuchagua moja kati ya kucheza mpira na kubakishwa kambini au awafuate kina Meddie Kagere, Chris Mugalu na Taddeo Lwanga waliofyekwa Misri.
Inadaiwa Bocco amekuwa akitegea sehemu ya mazoezi ya timu na inadaiwa imemfanya kocha huyo kukaa naye na kumtaka achague kucheza au kama anasumbuliwa na majeraha basi atafutiwe matibabu haraka kabla ya kufanya uamuzi wa kubaki naye Msimbazi au kufyekwa kama alivyofanywa kwa kina Mugalu waliorejeshwa nchini.
Katika hatua nyingine kocha huyo amesisitiza anataka atafutiwe washambuliaji wawili akiwamo namba tisa wa ukweli kutokana dili na Cesar Manzoki kuonekana kukwama na kusubiriwa kuongezwa katika dirisha dogo, jambo litakaloifanya timu isiwe na straika wa kutegemewa.
Awali, ilitarajiwa dili la Manzoki likamilishwe kwa Simba kutuma kigogo kwenda kuzungumza na uongozi wa Vipers ya Uganda inayommiliki mchezaji huyo, lakini mambo yamekwama kwa sababu klabu hiyo ya Uganda inataka ilipwe Dola 200,000 miezi miwili iliyobaki ya mkataba wake.