Dirisha la usajili liko wazi hadi Agosti 31 huku klabu mbalimbali zikiendelea kuboresha vikosi vyao kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano mbalimbali.
Licha ya kila timu kufanya usajili mkubwa ila Mwanaspoti linakuleta makala ya baadhi ya wachezaji ambao mashabiki wanategemea makubwa kutoka kwao.
Moses Phiri (Simba)
Nyota huyo ametokea Zanaco ya Zambia. Amejiunga na Simba akitokea kufunga mabao 14 katika Ligi Kuu ya Zambia akiwa wa pili nyuma ya mfungaji Bora wa msimu, Ricky Banda aliyemaliza na mabao 16.
Phiri anatazamiwa kufanya makubwa kutokana na uwezo wake wa kufunga jambo ambalo lilikuwa changamoto kwenye kikosi hicho msimu uliopita.
Stephane Aziz Ki (Yanga)
Alijiunga na mabingwa hawa wa Ligi Kuu Bara akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast ukiwa ni usajili uliotikisa kutokana na utambulisho wake.
Raia huyu wa Burkina Faso alitambulishwa Julai 15, saa 9:00 alasiri ukiwa ni usajili uliotikisa nyoyo za mashabiki ambao wanategemea makubwa kutoka kwake.
Augustine Okrah (Simba)
Inatajwa kama moja ya sajili zilizovunja benki kwenye kikosi cha Simba ni wa Okrah aliyetokea klabu ya Bechem United ya kwao Ghana.
Okrah aliyefunga mabao 14 na kutoa asisti tatu msimu ulioisha, tayari ameanza kuonyesha ni mchezaji anayebeba matumaini makubwa ya kutokana na kiwango bora anachokionyesha kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo mji wa Ismailia, Misri tangu Julai 14.
Ali Ahmada (Azam FC)
Eneo la golikipa ni sehemu ambayo imekuwa changamoto kubwa kwa Azam tangu alipoondoka Aishi Manula na kujiunga na Simba 2017.
David Kissu, Mwadini Ally, Razack Abarola, Benedict Haule na Mathias Kigonya ni miongoni mwa makipa walioshindwa kuwika hali iliyowafanya mabosi kuvunja benki na kumsajili Mcomoro, Ahmada ambaye pia ni mzaliwa wa Ufaransa kutibu tatizo hilo.
Ahmada (30) ni mzoefu na aliwahi kucheza klabu mbalimbali barani Ulaya, ikiwemo Toulouse ya Ufaransa inayoshiriki Ligue 1.
Yusuph Mhilu (Kagera Sugar)
Mhilu alijiunga na Simba mwaka jana ila kutokana na kushindwa kuonyesha ubora uliomleta imemfanya kurudishwa tena Kagera Sugar alikotokea.
Kurudi kwake kunatoa matumaini makubwa kwa ‘Wanankurukumbi’ kuelekea msimu ujao kwani wakati anaondoka alifunga jumla ya mabao tisa.
Maabad Maulid (Coastal Union)
Baada ya kuondoka kwa Abdul Suleiman ‘Sopu’ aliyetimkia Azam, mabosi wa Coastal Union walinasa saini ya Maabad kutokea KVZ SC ya Zanzibar.
Nyota huyu anatazamiwa kubeba viatu vya ‘Sopu’ kwani msimu ulioisha aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Zanzibar kwa kufunga mabao 19 akiwa na kikosi hicho.
Gael Bigirimana (Yanga)
Sio rahisi kusikia mchezaji aliyechezea klabu kubwa duniani kama Newcastle United ya England anakuja kucheza kwenye ligi ya Tanzania.
Sio kwamba ligi yetu ndiyo dhaifu kuliko zote duniani, lakini kuna ugumu kwa nyota waliowahi kucheza levo zile kuja huku. Jambo hilo limetokea msimu huu baada ya raia huyu wa Burundi kujiunga na Yanga.
Wasifu wake ni vitu ambavyo vitamfanya kuangaliwa sana kwa kile atakachokionyesha akiwa na timu hiyo kwenye mashindano mbalimbali.
Obrey Chirwa (Ihefu)
Nyota huyo kutoka Zambia amejiunga na Ihefu akitokea Namungo huku akibeba matumaini kwa kikosi hicho kinachonolewa na Zubery Katwila kutokana na uzoefu wake wa kucheza timu kubwa zikiwemo Platinum, Azam na mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga.
Bernard Morrison (Yanga)
Maisha yake ya soka nchini aliyaanzia Yanga 2020 alikodumu kwa msimu mmoja uliotawaliwa na vituko visivyoisha kila uchao kisha kutimkia Simba katika mazingira ya utata. Yanga wakaenda Fifa wakidai alikuwa bado ana mkataba nao, akawashinda, akabaki zake Simba. Hata hivyo, Wekundu wa Msimbazi pia walishindwa kumvumilia na kumuacha kabla ya msimu uliopita haujaisha.
Msimu ujao raia huyo wa Ghana atavaa tena jezi za njano na kijani huku akisubiriwa ni kipi atakionyesha kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara.
MSIKIE BARESI
Aliyekuwa kocha mkuu wa JKT Tanzania, Mohamed Abdallah ‘Baresi’ anasema usajili wa msimu huu umeo-nyesha ni kwa jinsi gani klabu zimejipanga na kutotaka kurudia makosa ya msimu uliopita huku fedha za wadhamini zilizotoka zikichochea ushindani.
“Timu kama Coastal Union inaenda nje na kuleta wachezaji wakubwa wa kigeni, hili ungetarajia kuliona kwa Simba, Yanga na Azam FC tu ambazo zina huo uwezo, lakini mara hii timu nyingi zimefanya hivyo, jambo ambalo linaashiria soka letu limepiga hatua,” alisema Baresi.