Home Habari za michezo KWA USAJILI WA SIMBA NA YANGA…KWENYE MECHI ZA WATANI ATAKAYEZUBAA TU IMEKULA...

KWA USAJILI WA SIMBA NA YANGA…KWENYE MECHI ZA WATANI ATAKAYEZUBAA TU IMEKULA KWAKE ASUBUHI NA MAPEMA…


Mtaani mashabiki wa Yanga na Simba wanatamba kwamba kila upande umefanya usajili kiboko ambao utakomesha upande wa pili pindi timu zao zitakapokutana pia kuwapa heshima ya mataji msimu ujao, wakianza na mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Agosti 13.

Timu hizo ziotakutana kwenye pambano hilo la kuzindua msimu wa 2022-2023 wa Ligi Kuu Bara itakayoanza siku nne baadaye.

Hata hivyo, tathmini ya umri wa safu za ulinzi na ushambuliaji za timu hizo mbili iliyofanywa , imebaini kuwa mchezo baina ya timu hizo mbili huenda ukahitaji hesabu na nidhamu kubwa kwa kila upande ili uweze kuvuna ushindi vinginevyo ukijichanganya utabaki na kilio.

Usajili ambao Simba na Yanga zimefanya katika dirisha kubwa linaloendelea la uhamisho wa wachezaji, umefanya kuwe na uwiano unaokaribiana wa umri baina ya safu zao za ushambuliaji na ulinzi ambao utasaidia kila upande kwa uzoefu lakini pia nguvu na kasi katika idara hizo muhimu.

Safu ya ushambuliaji ya Simba ambayo inaonekana kuwa na umri mdogo itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya safu ya ulinzi ya Yanga ambayo nayo inaonekana kutokuwa na umri mkubwa na kinyume chake, Simba ina safu ya ulinzi yenye umri mkubwa ambayo itakuwa na kibarua dhidi ya safu ya ushambuliaji ya Yanga yenye umri mkubwa kwa wachezaji wake.

Yanga ambayo katika dirisha hili la usajili imewaongeza washambuliaji Bernard Morrison na Lazarous Kambole na kufanya idadi ya wachezaji wa idara hiyo kufikia tisa, wastani wa umri wa washambuliaji wake ni miaka 27.7 ambao watalazimika kuipenya safu ya ulinzi ya Simba ambayo wastani wa umri wa mabeki wake ni miaka 27.3.

Morrison ndiye mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi katika safu ya ushambuliaji ya Yanga akiwa na umri wa miaka 29, ila ukiondoa yeye, wapo pia Fiston Mayele, Heritier Makambo na Lazarous Kambole ambao kila mmoja ana umri wa miaka 28.

Lakini Yanga ina silaha za ziada za washambuliaji wenye umri mdogo ambazo ni Denis Nkane mwenye miaka 18, Yusuph Athuman (22), Ducapel Moloko (24), Dickson Ambundo (26) na Crispin Ngushi mwenye umri wa miaka 25.

Safu hiyo ya ushambuliaji ya Yanga kama inajivunia uzoefu kutokana na ukubwa wa umri wao, itapaswa kuipa kipimo safu ya ulinzi ya Simba ambayo inaundwa na wakubwa wenzao ambao hawapishani sana kwa wastani wa umri.

Katika kundi la mabeki tisa ambao wamesajiliwa na Simba kwa msimu ujao, Erasto Nyoni ndiye mkongwe zaidi akiwa na miaka 34 ambaye uwepo wake unafanya timu hiyo kuwa na wachezaji watano ambao wana umri wa zadi ya miaka 28.

Mbali na Nyoni, kuna Kennedy Juma (28), Joash Onyango (29), Enock Inonga (28) na Shomari Kapombe mwenye miaka 30.

SOMA NA HII  BAADA YA CHAMA KUSEPEA ZAKE YANGA....HII HAPA MASHINE INAYOKUJA KUMRITHI SIMBA...

Ikiwa kasi ya wapinzani itaonekana kuwaelemea wakongwe hao, wanaoweza kuwapa sapoti ni Nasoro Kapama mwenye umri wa miaka 27, Mohamed Hussein (25), Mohamed Ouattara (23) na Israel Mwenda (22).

Kwa upenda wa safu ya ulinzi ya Yanga ambayo wastani wa umri wa wachezaji wake ni miaka 24.3 watakutana na vijana wenzao wa safu ya ushambuliaji ya Simba yenye wastani wa umri wa miaka 25.6.

Nyota wa Simba wanaounda safu ya ushambuliaji na umri wao kwenye mabano ni Moses Phiri (29), Peter Banda (21), Cesar Manzoki (25) ambaye hata hivyo usajili wake umekwama kwa sasa hdi Desemba, Augustine Okrah (28), Pape Sakho (25), Jimmyson Mwanuke (23), Habib Kiyombo (21) na John Bocco (33).

Yanga yenyewe, safu yao ya ulinzi msimu huu itakuwa na nyota tisa ambao kila mmoja na umri wake kwenye mabano ni Dickson Job (21), Yannick Bangala (28), Abdallah Shaibu (23), Ibrahim Baka (22), Bakari Mwamnyeto (26), Joyce Lomalisa (29), Shomari Kibwana (21), David Bryson (20) na Djuma Shaban mwenye miaka 29.

Kwa upande wa Azam FC ndio timu ambayo ina kundi kubwa la wachezaji wenye umri mdogo katika safu za ushambuliaji na ulinzi wakizipiga bao, Simba na Yanga.

Wastani wa umri kwa safu ya ushambuliaji ya Azam FC ni miaka 24.2 wakati wastani wa umri kwa safu yao ya ulinzi ni miaka 23.2.

Hii ni kuonyesha kuwa timu hizo siku zikukutana zenyewe kwa zenyewe kazi itakuwepo kwelikweli kati ya safu za ushambuliaji na ile ya mabeki kwa wastani wa umri wao, ingawa soka ni dakika 90.

WASIKIE WADAU

Nyota wa zamani wa Simba, Mussa Hassa ‘Mgosi’ alisema kuwa usajili uliofanyika msimu utaleta ushindani mkubwa baina ya SImba, Yanga na Azam.

“Ukiangalia Simba na Azam zilikuwa na changamoto katika safu ya ushambuliaji msimu uliopita na sasa zimefanya usajili wa wachezaji wazuri katika eneo hilo wakati huo Yanga nao imeongeza watu pale mbele.”

“Lakini pia kila timu imejiimarisha kwenye safu ya ulinzi hivyo ushindani baina yao naamini utakuwa mkubwa na vita ya ubingwa haitokuwa rahisi,” alisema Mgosi.

Nyota wa zamani wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ alisema anaamini timu yake itaendelea kufanya vizuri licha ya washindani wake Simba na Azam kuimarisha vikosi vyao.

“Yanga ilikuwa bora msimu uliopita na sasa hivi imefanya usajili mzuri wa wachezaji wazuri hivyo watakuwa bora zaidi kulinganisha Simba na Azam ambazo zimefanya usajili wa kutengeneza timu zao,” alisema Mmachinga.