Home Habari za michezo AMA KWELI SOKA LINALIPA….BAADA YA WYDAD KUMLIPA BIL1.6 ZAKE…WAARABU WENGINE KUMLIPA MSUVA...

AMA KWELI SOKA LINALIPA….BAADA YA WYDAD KUMLIPA BIL1.6 ZAKE…WAARABU WENGINE KUMLIPA MSUVA BIL1.1 KIULAINIII…


Ukisikia kufuru ndio hii sasa. Sio siri tena, hatimaye mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva amejiunga na Al-Qadsiah FC ya Saudi Arabia ambako atakuwa akilipwa Dola 500,000 kwa msimu, zaidi ya Sh1.1 bilioni.

Huyo ndiye Msuva ambaye siku chache zilizopita baada ya kuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi saba, alishinda kesi yake dhidi ya wajiri wake wa zamani Wydad Casablanca na anatarajiwa kulipwa Dola 700,000 ambazo ni zaidi Sh1.6 bilioni.

Wiki iliyopita Msuva alitua Saudi Arabia kifua mbele kwa ajili ya kukamilisha usajili wa kujiunga na Al-Qadsiah inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambayo ni maarufu kama Yelo Ligi na ataungana na mshambuliaji wa DR Congo, Walter Bwalya ambaye alitua kwa vigogo hao kwa mkopo msimu mmoja akitokea Al Ahly.

Nje ya Bongo imepata nafasi ya kufanya mahojiano maalumu na Msuva akiwa jijini Khobar yalipo maskani ya chama lake jipya na kueleza namna alivyoyaanza maisha yake mapya huko Saudi Arabia kwa Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud.

“Niko poa na nilipokewa vizuri tangu ile siku ambayo nimetua hapa Saudi Arabia, nina uzoefu wa kutosha kwa kukaa kwenye nchi za watu kwa miaka mingi sasa, hivyo sidhani kama mazingira yanaweza kuwa tatizo kwangu, mpira umenifanya kutembea nchi nyingi zenye hali tofauti ya hewa, hilo sio tatizo kwangu

“Kila kitu kimeenda vizuri kama nilivyotarajia kilichobaki kwa sasa ni kufanya kazi, bahati nzuri hii timu ina wachezaji ambao wanatoka Afrika kwa hiyo najisikia kama vile nipo nyumbani, nina shauku ya kucheza ligi yao.”

Kuhusu ugeni wake kwenye ligi, Msuva amesema, “Siku zote mpira ni uleule kinachobadilika ni ushindani na mbinu za kocha, nimefundishwa na makocha wengi na nimekuwa nikijtahidi kuendana nao, naamini nitafanya vizuri hapa.”

Mkataba ambao amesaini Msuva na Al-Qadsiah FC una kipengele cha kuongeza mwaka mwingine ikiwa atafanya vizuri na klabu hiyo ya daraja la kwanza.

Kwa nini Saudi Arabia na sio Ulaya ambako wengi walikuwa wakitarajia? Msuva alisema mpira ni kazi yake, hivyo baada ya kesi yake na Wydad Casablanca kumalizika alitazama wapi kuna ofa nzuri zaidi licha ya kuwepo kadhaa kutoka huko.

SOMA NA HII  MAYELE AWEKA REKODI HII YANGA...APEWA JEZI YA HESHIMA...ISHU NZIMA IKO HIVI

“Ofa za Ulaya zilikuwepo ila tulitazama wapi ambako kulituvutia zaidi, ilituchukua muda kufanya maamuzi,” alisema mshambuliaji huyo.

Kuhusu kurejea nyumbani, “Nyumbani ni nyumbani, nilijiona bado ninaweza kuendelea kupeperusha bendera ya Tanzania nje ya nchi ndio maana nilizigomea ofa za Simba, Yanga na Azam FC, lakini nikiona imetosha ndio utakuwa mwisho nitarejea.”

“Itakuwa jambo zuri hata kwa familia yangu na mashabiki zangu kumalizia soka nyumbani. Siwezi kusema eti nitacheza soka hadi kustaafu kwangu nikiwa nje ya nchi hilo halipo, kuna siku sijui lini ila nitamalizia nyumbani na kupumzika.”

Licha ya kwamba Msuva alizigomea Simba, Yanga na Azam FC, anaziona mbali klabu hizo kwa kusema zinaweza siku moja kuliteka soka la Afrika lakini alikiri zina safari ndefu kulingana na uzoefu alioupata akiwa Wydad Casablanca ambayo msimu uliopita ilitwaa ubingwa wa Afrika kwa kuifunga Al Ahly ya Pitso Mosimane.

“Mpira wa Afrika una mambo mengi. Klabu zetu zinaonyesha zinaweza na hilo limethibitishwa misimu ya hivi karibuni. sasa zinatakiwa kuendeleza kutoka hapo na siku moja tunaweza kukiona kile ambacho kisichowezekana, naamini inawezekana,” anasema.

HII NDIO AL-QADSIAH

Kipindi cha mafanikio zaidi cha Al-Qadsiah aliyojiunga nayo Msuva katika historia kilikuja mapema miaka ya 90 iliposhinda Crown Prince Cup 1991-92 dhidi ya Al-Shabab kwa penalti 4-2 na kutwaa taji lake la kwanza.

Ushindi wa klabu hiyo uliiwezesha kufuzu kwa Kombe la Washindi wa Kombe la Asia. Ilitinga fainali kumenyana na China Kusini AA ambapo iliifunga kwa jumla ya mabao 6-2 na kutwaa ubingwa wa 1993-94.

Katika msimu huohuo pia ilitwaa Kombe la Shirikisho la Saudi 1993-94 kwa kuifunga Al-Nasser 2-0 kwenye fainali.

Baada ya misimu 21 mfululizo katika Ligi Kuu, pamoja na kufanikiwa kutwaa mataji mawili ya nyumbani na taji moja la bara, klabu hiyo ilishushwa daraja kwa mara ya kwanza katika historia yake katika msimu wa 1996-97.