Home Habari za michezo MZEE DALALI AIPELEKA SIMBA DAY CAF…ASIMULIA WALIVYOPATA MILIONI 70…ATIA NENO KUHUSU USAJILI...

MZEE DALALI AIPELEKA SIMBA DAY CAF…ASIMULIA WALIVYOPATA MILIONI 70…ATIA NENO KUHUSU USAJILI …


WAKATI uongozi wa Simba ukikiri kuchelewa kutambulishwa kwa jezi mpya ni tatizo, aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali amesema Tamasha la Simba Day kwa sasa limekuwa ni tukio la kimataifa barani Afrika tofauti na lilivyokuwa miaka ya nyuma.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amewataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuwa watulivu na wakae tayari kuzipata jezi mpya kabla ya Tamasha la Simba Day halijafanyika.

Ahmed alisema sababu kubwa iliyopelekea jezi kuchelewa ni mazungumzo ya kupata mdhamini mpya, lakini akasema jezi hizo ziko njiani.

Naye Dalali alesema kuwa kwa sasa maandalizi ya Simba Day yamekuwa makubwa na kupongeza weledi unaofanywa na viongozi walioko madarakani.

“Simba ya sasa sio ile ya mwanzo, viongozi wanaendeleza vyema tamasha hili, Simba Day ya kwanza ilifanyika mwaka 2009 na lengo lilikuwa kukusanya pesa kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo ya klabu ambapo tulipata Sh. milioni 70, kiasi kidogo kilitumika kupata Uwanja wa Bunju,” alisema Dalali.

Aliongeza anafurahi kuona viongozi wamefanya usajili bora na mechi za kirafiki zilizochezwa zitakuwa zimesaidia kuimarisha kikosi huku akiamini wataurudisha ubingwa wa ligi waliopokonywa na watani zao.

Kilele cha Simba Day kinatarajiwa kufikia keshokutwa ambapo mbali na zoezi la kutambulisha wachezaji wapya, timu yao itacheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya mabingwa wa Ethiopia, St. George wakati Simba Queens itawaalika Fountain Gate Princess kutoka jijini Dodoma.

Baada ya tamasha hilo, Simba itaendelea na mazoezi yake kwa ajili ya kuwakabili Yanga katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii itakayochezwa Agosti 13 na Agosti 17, mwaka huu itawakaribisha Geita Gold FC kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

SOMA NA HII  ALICHOSEMA MATOLA BAADA YA ISRAEL MWENDA KUCHEZA 'FYONGO' NYINGI JANA...ATUPA LAWAMA KWA WOTE...