KUELEKEA mechi ya kuwania Ngao ya Jamii itakayowakutanisha watani wa jadi nchini, Yanga na Simba, makocha wa timu hizo wameendelea kutamba vikosi vyao vimeimarika, lakini kila upande ukijiandaa kuzidisha umakini ili kuhakikisha wanatimiza malengo ya kuondoka na ushindi katika mchezo huo.
Yanga inatarajia kuikaribisha Simba katika mechi hiyo ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2022/2023 itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amewataka wachezaji wake kucheza kwa kujituma zaidi ili kufikia malengo ya kuwafunga wapinzani wao, Simba ambao pia wanaonekana ni wenye ubora.
Nabi alisema kiwango kilichoonyeshwa na Simba katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Tamasha la Simba Day dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu Ethiopia, St. George lilimpa mwangaza mahali ambapo wapinzani wao walipo.
“Utakuwa mchezo mgumu na wenye changamoto mbalimbali, kila timu ina wachezaji wazuri, wenye uzoefu lakini wenye kiu ya kupata matokeo bora, ili ufikie huko ni lazima tuwe watulivu na tucheze kwa tahadhari wakati wote,” alisema Nabi.
Taarifa kutoka katika kambi ya Yanga zinasema Nabi amefanya kikao na wachezaji wake na kuwataka wawe makini katika mchezo huo kwa sababu Simba ni timu ngumu.
“Kocha Nabi amewataka wachezaji wajitume katika mazoezi ili wahakikishe wanaibuka na ushindi Jumamosi, amesema anaijua Simba ni timu nzuri na ngumu kutokana na alivyoiona katika mechi yake dhidi ya St.George, anaiheshimu, anasisitiza zaidi wachezaji utulivu ingawa anakiamini kikosi chake kinaweza kupata ushindi katika mchezo huo,” kilisema chanzo chetu.
Kiliongeza mabosi wa timu hiyo wakiongozwa na Rais, Injinia Hersi Said, leo wanatarajia kukutana na wachezaji ili kutoa ahadi yenye lengo la kuwaongezea hamasa kuelekea mchezo huo.
Naye Kocha Mkuu wa Simba, Zoran Maki, aliliambia gazeti hili wachezaji wake wako tayari kuwakabili wapinzani wao na amekamilisha hesabu za kuelekea mechi hiyo muhimu.
“Tumefanya kila kitu muhimu, tunaamini tutapata matokeo mazuri, wachezaji wangu wanaendelea kunivutia kila siku, ninaamini hawatawaangusha mashabiki wao,” alisema Maki.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema wanajivunia kuwa na kikosi imara.
“Dabi ni mchezo usiotabirika, tunawaheshimu Yanga, lakini kwa sasa tuna timu nzuri kuliko wao, mechi tofauti sana, lakini tumejipanga kushinda,” Try Again alisema.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema litachukua tahadhari zote za kiusalama kabla, wakati na baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii ili kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.
Kamanda wa Kanda Maalum, Jumanne Muliro, alisema wamejipanga kuhakikisha usalama unakuwa wa kiwango cha juu huku akiongeza hakutakuwa na mtu au kikundi chochote kitakachoruhusiwa kuingia na silaha ya aina yoyote uwanjani.
Alisema Polisi watazingatia maadili, weledi na kuzitunza siri za wananchi huku akitoa wito kwa jamii kuimarisha mifumo ya ulinzi shirikishi ili kuzuia vitendo vya uhalifu.
Kamanda huyo amewaondoa hofu mashabiki wa soka wanaohofia kufika uwanjani kwa kuwaeleza ulinzi utaimarishwa kwa kiwango cha juu.