KIUNGO wa zamani wa Simba, Amani Mbaruku alilifuatilia pambano la watani la Ngao ya Jamii na kusema kocha wa Simba, Zoran Maki alikosea sana kumtoa Sadio Kanoute kwani ndiye aliyekuwa akikata kabisa umeme ulioidhoofisha Yanga katika mchezo wa juzi.
Yanga ilishinda 2-1 kupitia mabao ya Fiston Mayele yaliyopatikana baada ya Zoran kufanya mabadiliko ya kuwatoa kwa mpigo wachezaji watatu akiwamo Kanoute, Clatous Chama na Kibu Denis na kuwaingiza Augustine Okrah, Nelson Okwa na Mzamiru Yasin.
Mbaruku, aliyekuwa kwenye kikosi cha dhahabu cha Simba cha mwaka 2003 kilichoitoa Zamalek katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, alisema viungo wakabaji huwa kama hawaonekani katika mchezo lakini wana umuhimu mkubwa.
Alisema Simba ilikuwa inahitaji Kanoute kutokana na aina yake ya uchezaji ya kugongana kwani inawapunguza nguvu wapinzani.
“Dogo anajua sana kugonga, anagonga mno, ile ni sawa yule ni kiungo wa kazi na alikata mirija yote ya Yanga alimfanya Feisal Salum asicheze pamoja na Sure Boy alipotoka tu pale Yanga wakaanza kucheza na kutengeneza nafasi. Labda kocha alihofia anaweza kupata kadi ya pili ya njano.”