Wallace Karia ambaye ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) amesema kuwa watu wanaodai kuwa kanuni za maadili zilizomuadhibu aliyekuwa Msemaji wa Klabu ya Yanga, Haji Manara ni batili basi hata ubingwa wa msimu uliopita ni batili.
Karia amesema kanuni hizo ni halali kwani zimetungwa miaka mingi iliyopita lakini zimekuwa zikiboreshwa ili kuendana na mazingira na mabadiliko ya mifumo na uendeshaji wa ligi na soka kwa ujumla.
Karia amekanusha tuhuma hizo jana kwenye mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao kupitia zoom kujadili tathmini na matarajio ya wadau wa soka juu ya mwenendo wa usajili wa wachezaji kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya NBC 2022/2023.
“Ligi yetu ni miongoni mwa ligi nne ambazo zina hamasa kubwa Afrika, na sisi Tanzania tuna vivutio vikubwa duniani ambavyo wengine hawana na tuna Simba na Yanga ambazo wengine hawana.
“Sisi tuna nafasi ya kuboresha kanuni hizi kutokana na matukio yanayotokea au mabadiliko yanayotokea.
“Anayesema kanuni hazipo kihalali, kanuni hizo hizo ndio zinasema mwenye pointi nyingi awe bingwa, sasa kama mtu anasema kanuni hazipo kihalali ina maana ligi yetu ya msimu uliopita ilikuwa batili.
“Kuna kanuni ambazo zinahusu nidhamu na maadili, hizi tumezikopi kutoka FIFA tukaziongeza kidogo kutokana na mazingira, kwa mfano kanuni za maadili na nidhamu hizi zimetengezezwa zaidi ya miaka 9 iliyopita.
“Sisi tumechukua mfumo wa Hispania ndio maana Ngao ya Jamii itakuwa shindano la timu nne na hayo maamuzi tuliyafanya kwenye kikao cha kamati tendaji Arusha kabla ya kumalizika kwa msimu,” amesema Karia.