Kuelekea Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza, Kocha Mkuu wa Nyasa Big Bullets, Kalisto Pasuwa, amefichua kuwa kwa sasa amekuwa akiwafuatilia kwa karibu wachezaji wa Simba kupitia video za mechi mbalimbali akiwemo Mzambia, Clatous Chama na Pape Sakho, raia wa Senegal kabla ya mchezo wao.
Simba inatarajia kucheza mchezo hatua ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi Septemba 9, mwaka huu nchini Malawi kabla ya mchezo wa marudiano Septamba 16, mwaka huu kwenye dimba la Mkapa, Dar.
Pasuwa alisema kuwa kwa sasa amekuwa akiwafuatilia baadhi ya wachezaji wa Simba ambao wanaonekana kuwa tishio kabla ya mchezo huo kwa lengo la kujiandaa kupambana nao.
“Nadhani kitu cha msingi kwetu ni kuwapa heshima yao kwa sababu za wao kuwa na uzoefu mkubwa na michuano hii lakini siyo kuogopa kwa sababu hata upande wetu malengo yetu ni kuhakikisha tunafika katika hatua za juu katika michuano hii.
“Simba inawacheza wa wazuri na wakubwa ambao wanapaswa kuchungwa muda wowote kwa sababu wana uwezo wa kukuadhibu wakati wowote, ndiyo maana tunajaribu kuwafuatilia katika baadhi ya video za mechi zao kabla ya kukutana nao kwa kuwa naamini itatusaidia kufikia malengo yetu,” alisema Pasuwa.