RAUNDI ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ilimalizika juzi huku jumla ya mabao 20 yakifungwa, ikizaa penalti nne na kutengeneza rekodi ya aina yake ambayo haijawahi kutokea.
Hakuna rekodi yoyote huko nyuma inayoonyesha kupatikana kwa penalti nne kwenye mechi za raundi ya kwanza tu ya Ligi Kuu.
Idadi hiyo ya mabao msimu huu imeongezeka kwa asilimia 100 kwani kwenye mechi za raundi ya kwanza msimu uliopita mabao 10 tu yalifungwa.
Mabao 20 yaliyopatikana kwenye mechi za ufunguzi wa ligi msimu huu, yalipatikana kwa Ruvu Shooting ikiwa ugenini, Highland Estate, Mbarali mkoani Mbeya kuifunga Ihefu bao 1-0, Namungo kulazimishwa sare ya mabao 2-2 Benjamin Mkapa, Dar es Salaam dhidi ya Mtibwa Sugar, Singida Big Stars ikiidungua Prisons bao 1-0 kwenye Uwanja wa Liti Singida, na Yanga ikiwa ugenini Shekh Amri Abeid Arusha ikiichapa Polisi Tanzania mabao 2-1.
Dodoma Jiji ikiwa nyumbani Uwanja wa Liti Singida, ilikiona cha moto kwa kubamizwa mabao 3-1, Coastal Union ikiwa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ikishinda bao 1-0 dhidi ya KMC, wakati Simba ikiisasambua Geita Gold mabao 3-0, na mechi ya mwisho ya raundi hiyo, iliishuhudia Azam FC ikitoa kipigo cha mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex dhidi ya Kagera Sugar.
Jumla ya penalti nne zimepatikana zikiwa ni nyingi zaidi kutolewa kwenye historia ya ligi hiyo kwenye raundi ya kwanza.
Simba na Yanga nazo zimeingia kwenye rekodi ya timu zilizobahatika kupata penalti kwenye mechi za ufunguzi wa Ligi Kuu.
Hata hivyo, mbili ziliwekwa wavuni na zilizobaki zilikoswa, Namungo ndiyo timu iliyoanza kupata penalti msimu huu, lakini mpigaji wao, Ibrahim Ally kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar alikosa, huku Fiston Mayele naye akikosa penalti ambayo Yanga ilizawadiwa kwenye mechi dhidi ya Polisi Tanzania.
Penalti mbili zilizowekwa wavuni ni zile zilizopatikana kwenye mechi kati ya Coastal Union dhidi ya KMC, Amza Moubarack raia wa Cameroon akifunga bao pekee lililoipa ushindi Coastal, na Mzambia Clatous Chama akiitendea haki penalti ya nne iliyopatikana kwenye raundi ya kwanza, akiifungia Simba bao kwenye mechi ambayo walishinda mabao 3-0 dhidi ya Geita Gold.