Home Habari za michezo LIGI KUU NBC…AZAM WAANZA KUMPIGISHA ‘SHOTI’ BILIONEA BAKHRESA….WABRAZILI WAIOKOA SINGIDA BIG STARS…

LIGI KUU NBC…AZAM WAANZA KUMPIGISHA ‘SHOTI’ BILIONEA BAKHRESA….WABRAZILI WAIOKOA SINGIDA BIG STARS…


Matajiri wa Chamazi, Azam FC wamelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Geita Gold katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Azam FC ilitangulia kwa bao la chipukizi wake mwenye kipaji, Tepsie Evans dakika ya 41, kabla ya beki Adeyoum Ahmed kuisawazishia Geita Gold dakika ya 54.

Ni sare ya kwanza kwa timu zote katika mechi mbili za mwanzo za msimu kufuatia Azam FC kushinda 2-1 dhidi ya Kagera Sugar hapo hapo Chamazi na Geita Gold kufungwa 3-0 na Simba Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo wa mapema jana Klabu ya Singida Big Stars imeendeleza wimbi la ushindi kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Liti mkoani Singida.

Mbeya City ilikuwa ya kwanza kupata bao la utangulizi kupitia kwa mshambuliaji wake, Sixtus Sabilo baada ya kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Singida Big Stars, Metacha Mnata.

Dakika ya 53, Singida ilipata bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti kupitia kwa Dario Feredrico baada ya nyota huyo kuangushwa kwenye eneo la hatari na kipa wa Mbeya City, Haroun Mandanda.

Baada ya hapo Singida iliendelea kulishambulia lango la wapinzani wake na kunako dakika ya 61, Bruno Gomes aliiandikia bao la pili na la ushindi na kuifanya timu hiyo kushinda michezo yake yote miwili ya mwanzo.

Ushindi huo unaifanya kufikia pointi sita ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa Agosti 16 kuifunga Tanzania Prisons bao 1-0.

Kwa upande wa Mbeya City inasalia nafasi ya sita na pointi zake tatu kufuatia mchezo wa kwanza dhidi ya Dodoma Jiji uliopigwa Agosti 17 kushinda mabao 3-1.

SOMA NA HII  WIKIEND YA KIPUTE CHA 'MIHELA' INAANZA KESHO....KAMATA ODDS ZA USHINDI KUPITIA MERIDIANBET..