Mashabiki wa Yanga hadi sasa hawajajua kikosi cha kwanza hasa eneo la beki wa kati kutokana kocha Nassredine Nabi kumrudisha Yanick Bangala na kuwapa changamoto Bakari Mwamnyeto na Dickson Job, lakini taarifa ni kwamba wote watacheza.
Nabi ameeleza wote ni wachezaji wazuri na watacheza kutokana na mechi husika kwani kila mmoja ana sifa na msaada wa aina yake kikosini.
“Wote ni bora na kila mmoja ana sifa yake, lakini kama ulivyoona kikosini kuna watu wameongezeka hivyo kutakuwa na mabadiliko,” alisema Nabi.
“Pamoja na mabadiliko hayo, lakini wote wataendelea kucheza kutokana na mbinu za mechi husika kwani kila mmoja ana upekee wake na sio hao tu bali wachezaji wote wa Yanga watapata nafasi kutokana na ubora wao.”
Kiungo wa zamani wa Yanga na Simba, Amri Kiemba ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka aliwataka mashabiki wanaowalingaisha wachezaji hao wawili kuwapa heshima kwani kila mmoja ni bora na ana mchango mkubwa kwa timu hiyo.
“Wachezaji hao hawapaswi kutafutiwa kushindanishwa, bali wapewe heshima wanayostahili kwani kila mmoja ana mchango wake kwenye timu,” alisema “Job anajijua ni mfupi, hivyo anakuwa makini kucheza mipira ya juu anayohisi akichelewa itakuwa na madhara. Pia ni bora kuanzisha mashambulizi na kumiliki mpira na hizo ndio sifa zake kuu.
Nabi atakuwa na machaguo matano ya beki wa kati kwa kuwatumia Job, Mwamnyeto, Bangala, Ibrahim Bacca na Abdallah Shaibu.