Wakati Simba ikiendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa Vipers ya Uganda, kuhusu kukamilisha mpango wa kumsajili rasmi mshambuliaji Cesar Manzoki, mwenye uraia wa DR Congo na Afrika ya Kati, nyota huyo mkali wa kucheka na nyavu, ametua kimyakimya jijini Dar es Salaam.
Nyota huyo aliingia nchini juzi usiku ikidaiwa kwamba ujio wake ni baada ya Simba kukubali kutoa ada inayokadiriwa kuwa Sh. milioni 233 ambazo Vipers imelazimika kukubali kiasi hicho badala ya Sh. milioni 400 ilizokuwa ikitaka awali, hiyo ikitokana na Manzoki kugoma kuichezea.
Kwa mujibu wa Gazeti la Nipashe, nyota huyo yuko nchini tangu juzi usiku na amejichimbia katika moja ya hoteli jijini Dar es Salaam na huenda akawa sehemu ya kikosi kitakachoelekea Sudan kesho kwa mechi za kirafiki kama mambo yatakwenda sawa kati ya Simba na waajiri wake wa zamani, Vipers.
“Kuhusu suala la Manzoki, mashabiki wakae kwa kutulia kwa sababu (muda utaongea) ni mchezaji wa Simba na yupo hapa toka juzi ana mambo yake anafanya, alisema mtoa habari huyo.
Kuhusu nani atatemwa kumpisha kinara huyo wa ufungaji wa Ligi Kuu Uganda msimu uliopita, mtoa habari wetu alisema suala hilo liko chini ya Kocha Mkuu, Mserbia Zoran Maki.
“Kwa sasa hatutaki kuingilia mapendekezo ya benchi la ufundi, anaposema tunahitaji mchezaji fulani, basi tunatekeleza mahitaji yake kulingana anachokihitaji kikosini kuelekea michuano iliyopo mbele yetu, nani atampisha Manzoki hilo ni juu ya kocha mwenyewe alisema.
Kwa mujibu wa Meneja ldara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema suala la Manzoki bado wanalifuatilia na wako katika mipango mizuri ya kufanikisha kupata saini ya nyota huyo. Alisema bado hawajamalizana na Vipers, lakini mazungumzo yanaendelea kuhakikisha wanafanikiwa kumpata mchezaji huyo kwa ajili ya kuimarisha safu ya ushambuliaji.
“Manzoki ni mchezaji halali wa Vipers na bado ana mkataba, Simba tumejaribu kumfanya mazungumzo na klabu yake, lakini mambo hayajawa vizuri, ila bado tunaendelea na harakati za kumpata nyota huyo alisema Ahmed.
Kikosi cha Simba kikiwa bila wachezaji wanane walioitwa kuitumikia Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), kesho kitakwea pipa kuelekea Sudan kushiriki michuano maalum ya kujiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika iliyoandaliwa na Mabingwa wa nchi hiyo, Al Hilal.
Katika michuano hiyo, Simba itacheza mechi mbili ambapo Jumapili wiki hii itaanza kwa kuivaa Asante Kotoko ya Ghana kabla ya Agosti 31, mwaka huu kuvaana na wenyeji, Al Hilal.
Baada ya mechi hizo, Simba itarejea Dar es Salaam na kucheza mechi moja kimataifa ya kirafiki dhidi ya AS Arta Solar 7 ya Djibouti, ambayo nayo imeweka kambi hapa nchini kujiandaa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.