Kipa Juma Kaseja amebainisha mipango yake kisoka akieleza kwamba yuko tayari kucheza kwenye timu yoyote itakayomhitaji hata kama ni ya daraja la kwanza.
Kaseja ambaye mkataba wake na KMC umemalizika msimu uliopita amesema hana fikra za kustaafu soka kwa sasa, ikitokea timu inahitaji huduma yake wakaafikiana atacheza.
“Sina timu kwa sasa, baada ya mkataba wangu na KMC kumalizika niliendelea na maisha mengine, lakini kwa kuwa furaha yangu ni kucheza mpira, naendelea kujifua na timu itakayonihitaji tukielewa nitacheza hata ikiwa ya daraja la kwanza,” alisema kipa huyo.
Kaseja aliyewahi kuzitumikia pia Simba, Yanga na Taifa Stars kwa mafanikio alisema yeye ni mchezaji na hafikirii kustaafu soka hivi karibui.
“Watu wengi walikuwa hawataki kuamini kama sipo tena KMC, walipotangaza kikosi chao jina langu halikuwepo, kwa kuwa mkataba wangu ulikuwa umekwisha niliendelea na maisha mengine, kwa sasa ni mchezaji huru,” alisema Kaseja, supastaa wa zamani wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
Alisema kama atapata timu kabla ya dirisha la usajili kufungwa mwishoni mwa mwezi huu, basi atasajili na kuendelea kuonekana kwenye Ligi nchini.
“Nitacheza timu yoyote itakayonihitaji, kama nilivyosema hata iwe ya daraja la kwanza, tukiafikiana nitacheza,” alisema kipa huyo aliyewahi kuitwa Tanzania one kutokana na kipaji chake.
Alisema kuna mambo mengi watu wamekuwa wakimuuliza kuhusu timu yake ya KMC lakini ameebainisha kwamba kila kinachotokea katika maisha hayo ndiyo maisha, hayapaswi kukatisha ndoto zako.