Kikosi cha Taifa Stars kinaendelea kujifua kwa ajili ya pambano la kwanza la raundi ya pili ya kuwania Fainali za CHAN 2023, huku kocha mkuu, Kim Poulsen akisema ana matumaini makubwa ya kushinda dhidi ya Uganda The Cranes nyumbani Jumapili.
Kocha Poulsen alisema pambano hilo sio mchezo mwepesi ila maandalizi yaliyofanyika hadi sasa yanawapa matumaini makuibwa ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo kabla ya kurudiana Sept 3.
“Morali ya wachezaji ni kubwa, ikionyesha jinsi gani kila mmoja wao anataka kupata nafasi ya kucheza, sio mchezo mwepesi kutokana na rekodi za wapinzani wetu, ila naamini tutafanya vizuri na kufikia malengo tuliyojiwekea,” alisema Kim na kuongeza;
“Abdul Suleiman ‘Sopu’ na Shomari Kapombe wanaendelea vizuri baada ya kupata majeraha madogo, hivyo kwa kushirikiana na benchi letu la ufundi na madaktari wamepewa programu binafsi ili kuhakikisha wanarejea kwenye hali zao za kawaida,” alisema.
Kwa upande wa kipa Aishi Manula alisema ugumu wa mchezo huo unatokana na kujuana na wapinzani wao vizuri kwani sio mara yao ya kwanza kukutana huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili kuipa sapoti timu ya taifa.
Stars ilifika hatua hiyo kwa kuing’oa Somalia kwa jumla ya mabao 3-1. Hii ni mara ya tatu kwa Stars na Uganda kukutana kwenye michezo ya kufuzu CHAN ambapo Stars imecheza fainali mbili 2009 na 2020 ilihali wapinzani wao wamefuzu fainali tano.
Mshindi wa jumla kati ya miamba hiyo atafuzu moja kwa moja.