Home Habari za michezo ‘TOM NA JERRY’ WA SIMBA SAKHO NA BANDA WALA KIAPO KUFANYA...

‘TOM NA JERRY’ WA SIMBA SAKHO NA BANDA WALA KIAPO KUFANYA BALAA…LEO KUKIWASHA DHIDI YA KATOKO SUDAN…


Simba tayari ipo kwenye ardhi ya Sudan kwa mwaliko wa wenyeji Al Hilal. Leo itashuka uwanjani kuvaana na Asante Kotoko ya Ghana kwenye michuano maalumu, huku mastaa wake Peter Banda na Pape Ousmane Sakho wakitamba watazitumia mechi hizo kurudi na moto katika Ligi Kuu Bara na mechi za CAF.

Simba iliondoka alfajiri ya juzi na nyota wake wote isipokuwa tisa waliopo Taifa Stars. Simba itacheza mechi mbili Sudan dhidi ya Kotoko kisha wenyeji wao Al Hilal kabla ya kurudi nchini kuvaana na Arta Solar ya Djibouti.

Banda na Sakho aliyeshinda bao bora la Afrika msimu uliopita wamekuwa machaguo ya kikosi cha kwanza cha Simba kwa sasa chini ya Kocha Zoran Maki na wameweka wazi kujipanga kufanya vizuri zaidi msimu huu ndani na nje ya nchi wakiwa ndani ya uzi wa Msimbazi.

Sakho amesema kuwa usajili uliofanywa na Simba katika dirisha kubwa umeongeza chachu ya upambanaji ndani ya timu pia uimara wa kikosi hivyo anaamini baada ya muda mfupi kikosi chao kitakuwa hakishikiki na wanaingia na hata wanaowabeza watatulia.

“Kwa kiasi kikubwa timu imebadilika sio kama ilivyokuwa msimu uliopita, wameongezeka wachezaji wapya wenye viwango bora wanaokuja kuongeza ushindani na morali ya kupambana zaidi,” alisema Sakho na kuongeza;

“Binafsi nimejipanga kufanya vizuri zaidi na kuwapa furaha wana Simba na niwatoe shaka tu kwani siku chache zijazo kikosi chetu kitakuwa hakizuiliki.”

Banda naye alifunguka ujio wa kocha na wachezaji wapya kubadili hali ya timu huku akitamba kukiwasha zaidi msimu huu.

“Msimu uliopita nilipata majeraha yaliyoniweka nje kwa muda hivyo kushindwa kuonesha kile nilichonacho kwa kiwango kikubwa, sasa niko fiti na naamini utakuwa msimu bora kwangu ndani ya Simba,” alisema nyota huyo wa timu ya taifa ya Malawi na kuongeza;

“Ukiangalia kikosi cha sasa unaiona Simba iliyojaa wapambanaji wenye mipango mikubwa, hatutaki kupoteza tena bali kufikia malengo tuliyojiwekea.”

Sakho na Banda walisajiliwa msimu uliopita ambapo walihitaji muda wa kuzoea mazingira na sasa wote kwa pamoja wameweka wazi kuwa tayari kwa kazi.

SOMA NA HII  ISHU NZIMA YA MKATABA WA MOLOKO HII HAPA...APINDUA MEZA KIBABE YANGA

Simba itarudi nchini mwanzoni mwa mwezi ujao kuendelea na Ligi Kuu ambayo hadi sasa inaongoza sambamba na maandalizi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikipangwa kuanzia hatua ya mtoano ya awali dhidi ya Nyassa Big Bullets ya Malawi ambayo Banda anaijua vizuri sana.