Home Habari za michezo KUELEKEA MSIMU MPYA….HENOCK INONGA AFUNGUKA NAMNA WATAKAVYOJENGA UKUTA WA ROMA KWA SIMBA…

KUELEKEA MSIMU MPYA….HENOCK INONGA AFUNGUKA NAMNA WATAKAVYOJENGA UKUTA WA ROMA KWA SIMBA…


Beki wa kati Simba na beki bora wa msimu uliopita, Henock Inonga amesema sio mtu anayependa kuongea zaidi awapo uwanjani, lakini kazi yake kubwa ni kuonyesha kiwango bora, huku akipiga mkwara “safari hii mtaona mavitu” yake.

Inonga amesema anaweza kuwa anafanya mzaha na masihara katika maeneo mengine, ila linapofika suala la uwanjani iwe katika mazoezi, mechi za mashindano au kirafiki hataki masihara na kazi yake.

Beki huyo amesema anawaheshimu wachezaji wenzake, benchi la ufundi, viongozi pamoja na wale wote waliohusika kumchagua kama beki bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita kwani haikuwa kazi rahisi kutokana na kuwepo wengine walio bora.

“Wakati nafika Simba nilitoka DR Congo na tuzo ya beki bora wa msimu, nikafika Tanzania. Nashukuru msimu wangu wa kwanza tu nimeweza kuitetea tena tuzo hiyo tena katika nchi nyingine,” alisema Inonga.

“Tuzo hii inakuwa kama deni kwangu. Natakiwa kupambana ili kuendelea kucheza katika kiwango bora katika mashindano yote ili kuweza kuisaidia timu yangu kufanya vizuri.

“Binafsi mara zote ninapokuwa uwanjani nahakikisha nafanya vizuri na kutimiza majukumu yangu kulingana na vile ambavyo makocha watakuwa wamenielekeza.

“Kile ambacho nilionyesha msimu uliopitiliza nitajitahidi kupambana tena zaidi msimu ujao kuonyesha ubora zaidi ya ule ili kufikia malengo ya timu na mengine, yangu binafsi yatakuja yenyewe.”

Katika hatua nyingine Inonga amesema kikosi msimu ujao kimekuwa na mabadiliko makubwa tofauti na msimu uliopita.

“Timu imezidi kuimarika hasa kwenye maandalizi haya ya msimu ujao. Kila mchezaji kwa nafasi yake amefanikiwa kuonyesha alicho nacho kulingana na majukumu ya nafasi yake,” alisema Inonga ambaye amekuwa na ushindani mkubwa kila anapokutana na Mkongomani mwenzake, straika wa Yanga, Fiston Mayele.

Katika hatua nyingine mbali ya uwepo wa Inonga na Joash Onyango kama mabeki wa kati wa kigeni wanaocheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza kocha Zoran Maki amemleta beki mwingine wa kigeni, Mohamed Ouattara.

Zoran alisema amefanya hivyo kwa ajili ya kuboresha safu yake ya ulinzi kwani Inonga, Onyango na Ouattara wote ni mabeki bora na wenye uwezo wa kufanya kazi vizuri.

SOMA NA HII  WAKATI SIMBA NA AZAM ZIKIVUMA KWA TETESI ZA USAJILI...MABOSI YANGA KUJA NA KISHINDO HIKI...

“Namfahamu Ouattara siku nyingi na nimewahi kufanya naye kazi huko nyuma katika timu tofauti na kufanikiwa kuchukua naye mataji -tena akiwa katika kikosi cha kwanza naamini uwepo wake hapa utaongeza uimara wa timu,” alisema Zoran.

“Mabeki hao watatu yeyote ambaye atakuwa katika kiwango bora nitampa nafasi ya kucheza kulingana na mechi husika, binafsi wote wamenivutia.”