Home Habari za michezo #SIMBADAY: MKUDE AWEKA REKODI YA KIBABE SIMBA…MAKOCHA 14 WAPITA NAYE JUU KWA...

#SIMBADAY: MKUDE AWEKA REKODI YA KIBABE SIMBA…MAKOCHA 14 WAPITA NAYE JUU KWA JUU…


Wakati mwingine vikosi B vya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, vinaweza kuchukuliwa poa, lakini akitazamwa staa wa Simba, Jonas Mkude anaweza akawapa nguvu ya kufanya jambo viongozi wa klabu hizo.

Mkude ni zao la Simba B sio tu huduma yake inainufaisha klabu yake, pia amekuwa mchezaji muhimu kikosi cha Stars.

Mwaka 2010 uongozi wa Simba uliwekeza nguvu kuviibua vipaji mbalimbali nchini, ndipo walitokea mastaa wengi akiwemo Mkude ambaye amekomaa Msimbazi hadi sasa.

Ameweka rekodi ya kucheza timu moja (Simba) ndani ya miaka 12, kikosi B miwili cha wakubwa 10.

Ufuatao ni uchambuzi wa Mkude kutokana na mchango wake ndani ya timu hiyo.

VIUNGO ALIOCHEZA NAO

Tangu Mkude alipopandishwa kutoka kikosi B 2011/12, amecheza na viungo wengi katika nafasi yake baadhi yake ni Mwinyi Kazimoto (huru), Said Ndemla, James Kotei (SBS), Thadeo Lwanga (Simba) na kiraka Erasto Nyoni (Simba).

Mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Yanga iliyochapwa mabao 5-0 na Simba, Mkude aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Kazimoto na huo ulikuwa mwanzo wa safari ya mafanikio yake ya soka.

Alianza kupewa na nafasi ya kucheza mara kwa mara na alionyesha uwezo mkubwa, unaompa uhakika wa kuwepo Simba hadi leo.

MATAJI ALIYOCHUKUA

Hadi sasa Mkude amechukua mataji ya Ligi Kuu Bara matano, 2012/13, 2018/19, 2019/20, 2020/21 na 2021/22, Wakati mataji ya ASFC alichukua 2016/2017, 2020/21 Kombe la Mapinduzi 2015 na 2022 pia yapo ya Ngao ya Jamii.

Mkude anasema anajisikia faraja kubwa kuchukua mataji hayo, anasisitiza anakuwa na kitu cha kukumbukwa ndani ya muda aliyocheza Simba.

“Natamani nichukue mengi zaidi, kwani ni timu iliyonilea tangu nikiwa mdogo hadi sasa, Simba ina historia na maisha yangu, ila kwa sasa siwezi kuzungumza sana,” anasema.

UTOVU WA NIDHAMU

“Ninapozungumziwa mtovu wa nidhamu, kiukweli sipendi na wanaponiambia mimi ni mlevi, wamezidisha, lakini mimi sipo hivyo, vinginevyo nisingekuwa mafanya vizuri uwanjani, soka linachezwa peupe,” anasema na kuongeza;

“Jambo lingine watu wanalotakiwa kulijua siyo lazima mimi nikawa nahodha, maana hakuna sehemu yoyote iliyoandikwa hivyo, kikubwa ni ufanisi wangu uwanjani.”

SIMBA DAY YA 9

Simba Day ya mwaka huu itakuwa ni ya tisa kwa Mkude, hivyo ni mchezaji pekee aliyelijua vyema tamasha hilo, jambo lililomfanya Bernard Morrison kumpa heshima yake kiungo huyo.

Msimu wa 2021/22 wakati Morrison anatambulishwa kwenye tamasha la Simba Day, alimtaja Mkude kama mchezaji pekee aliyedumu muda mrefu ndani ya kikosi kwamba anastahili heshima yake.

Ikiwa inasubiriwa Simba Day ya mwaka huu, Mkude alimposti Morrison kwenye mtandao wake wa kijamii (Instagram), akimbatanisha na maneno ya kufurahia kushiriki tamasha hilo kwa mara ya tisa.

SOMA NA HII  HUU MSHAHARA ANAOKULA NTIBAZONKIZA HAPO SIMBA SC..SIO POA..

KADUMU MIAKA 10

Kipaji na kiwango anachokionyesha ndani ya timu hiyo ni sababu ya Mkude kudumu Simba ndani ya miaka hiyo akitumika mara nyingi kwenye kikosi cha kwanza.

Makocha mbalimbali waliyopita kikosini hapo, wanakiamini kipaji cha Mkude, wakimtumia kama chaguo la kwanza, ingawa wakati mwingine anakuwa nje ya kazi, kutokana na mambo yake binafsi.

Aliyekuwa mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali anasema Mkude ni kati ya vijana wenye vipaji vikubwa, nje na hapo anaamini asingekuwa sehemu ya timu.

“Ni mchezaji pekee aliyepandishwa kikosi B aliyedumu na Simba kwa muda mrefu na anacheza kikosi cha kwanza, pongezi zangu zinakwenda kwa meneja Patrick Rweyemamu amefanya kazi kubwa ya kuwalea hao vijana,” anasema na kuongeza;

“Rweyemamu na wenzake waliyoshirikiana kusimamia vijana wa Simba B ya kina Mkude, Abdallah Seseme, Said Ndemla, Ramadhan Sing’ano, Edward Christopher na wengine wengi, walifanya kazi kubwa ya kuweka misingi imara kwa vijana.”

Rweyemamu anasema kazi yao ilikuwa kuibua vipaji, ila utayari unatakiwa kwa wachezaji wenyewe kuzingatia nidhamu ya kazi yao.

“Mchezaji anapaswa kujua soka lina ushindani mkali, vipaji vinazaliwa kila siku, hivyo anapopata nafasi anatakiwa kuiheshimu sana.”

MAKOCHA WALIOMFUNDISHA

Milovan Cirkovic (2011/ 2012), Patrick Liewig (2013), Abdallah Kibadeni (2013), Zdravko Logarusic (2013-2014), Goran Kopunovic (2014-2015), Dylan Kerr (2015-2016).

Wengine ni Jackson Mayanja (2016), Joseph Omog (2016-2017), Pierre Lechantre (2017-2018), Patrick Aussems (2018-2019), Sven Vandenbroeck (2019-2021), Didier Gomez (2021),Pablo Franco (2021/22) na Zoran Maki (2022/23).

Kibadeni ni kocha mzawa aliyemfundisha Mkude 2013, anasema faida ya matunda ya Mkude siyo tu kuinufaisha Simba, bali na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

“Si jambo la mchezo mchezaji kudumu Simba na Yanga zaidi ya miaka 10, kiukweli nampongeza sana Mkude kwa kutunza kipaji na kiwango chake, analotakiwa kulifanya ahakikishe mwisho wake ndani ya kikosi hicho unakuwa mzuri,” anasema.

ALIOCHEZA NAO

Edward Christopher ni kati ya wachezaji waliocheza nao kikosi B na timu ya wakubwa anasema, anajisikia faraja kuona Mkude kabaki kama nembo ya Simba.

“Tuliyopandishwa kipindi hicho tulikuwa na vipaji vya aina yake, huwa najisikia faraja kuona Mkude bado anaitumikia Simba kwa mafanikio ya juu, jamaa anajua mpira,” anasema.

Kwa upande wa Abdallah Seseme anayekipiga Kagera Sugar anasema; “Mkude alipandishwa dirisha kubwa sisi tulipandishwa dirisha dogo, nampongeza sana jamaa amepambana, kubakia Simba muda wote huo siyo jambo dogo.”