Home Ligi Kuu MCHEZO MZIMA NAMNA SIMBA ILIVYOBWANA MBAVU NA AZAM FC

MCHEZO MZIMA NAMNA SIMBA ILIVYOBWANA MBAVU NA AZAM FC

 


SASA ni rasmi kuwa Simba itamaliza viporo vyake vyote huku ikiwaacha wapinzani wao Yanga kuwa nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya jana kubanwa mbavu na Azam FC kwa kupata sare ya kufungana mabao 2-2.


Simba ilianza kupata bao la kuongoza dakika ya 27 kupitia kwa Meddie Kagere lilidumu mpaka kipindi cha pili ambapo mabingwa hao watetezi walijisahau na wakadhani wanacheza mchezo wa kirafiki.

Mambo yalikuwa magumu kipindi cha pili baada ya Azam FC kushtuka na kuwazidi ujanja Simba ambapo walipachika bao la kusawazisha dakika ya 67 kupitia kwa Idd Seleman huku wakiongeza lingine la haraka ndani ya dakika 9 kupitia kwa Ayoub Lyanga aliyepachika bao hilo dakika ya 76.

Shukrani kwa Luis Miquissone ambaye alipachika bao la kuweka mzani sawa ambalo liliwapa pointi moja Uwanja wa Mkapa dakika ya 78 kwa shuti kali akiwa nje ya 18.

Nyota wa mchezo ni kipa wa Azam FC, Mathias Kigonya ambaye aliokoa hatari tatu za wazi huku Clatous Chama akibaki kujilaumu mwenyewe baada ya kukosa penalti dakika ya 38.

Simba inafikisha jumla ya pointi 39 baada ya kucheza jumla ya mechi 17 ina mchezo mmoja mkononi huku Yanga ikiwa nafasi ya kwanza na pointi zake 44 ikiwaacha Simba kwa jumla ya pointi 5 ambapo hata ikishinda mchezo wake wa mwisho itafikisha pointi 42 na kudaiwa pointi mbili na Yanga iliyo kileleni.

Azam inafikisha jumla ya pointi 33 na imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa nafasi ya tatu baada ya kucheza jumla ya mechi 18.

Didier Gomes, Kocha Mkuu wa Simba alisema kuwa wachezaji walipambana ila walishindwa kutumia nafasi ambazo wamezitengeneza.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati alisema kuwa walihitaji ushindi ila walikwama kupata bao kipindi cha kwanza jambo lililowagharimu kupata pointi moja.

Licha ya Simba kusepa na pointi moja nyota wake wameongeza rekodi zao binafsi wakiwa ni namba moja, Kagere amefikisha bao la 9 akiwa ni kinara na Chama amefikisha pasi ya 9 akiwa ni mtengeneza nafasi namba moja Bongo.

SOMA NA HII  HII HAPA ORODHA YA WATUPIAJI BONGO

Stori na picha zaidi, ni ndani ya Championi Jumatatu