Kocha Msaidizi wa Timu ya taifa ya Tanzania ‘TAIFA STARS’ Mecky Mexime ametamba kuwa na uhakika wa kupambana vilivyo katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ dhidi ya Uganda.
‘TAIFA STARS’ itakua ugenini kesho Jumamosi (Septemba 03) katika jiji la Kampala kucheza dhidi ya Uganda, huku ikiwa na deni la kulipa kisasi na kushinda mchezo huo, baada ya kupoteza mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili (Agosti 28), kwa kipigo cha 1-0.
Mexime aliyeteuliwa na TFF sanjari na Kocha Mkuu Hanour Janza wakichukua nafasi ya Kocha Kim Poulsen, amesema kikosi chao kipo tayari kwa mchezo huo ambao utakua na ushindani mkubwa, huku akitaja sababu za kuwa na matumaini ya kufanya vizuri.
Amesema kuongezwa kwa Nahodha na Mshambuliaji wa Simba SC katika kikosi cha Taifa Stars John Bocco, kumeongeza kitu kwa wachezaji wengine ambao walikuwepo tangu katika mchezo uliopita dhidi ya Uganda.
Amesema Mshambuliaji huyo ana sifa ya kipekee ya kupambana Kimataifa na kupata mafanikio akiwa na klabu yake ya Simba SC, hivyo ameongeza morari kwa wenzake ambao pia wana matumaini makubwa kuelekea mchezo wa kesho Jumamosi.
“Uwepo wa John Bocco katika kikosi cha Taifa Stars umeongeza morari ya kutosha kwa wachezaji wenzake kutokana na uzoefu alionao katika Michuano ya Kimataifa, tunaamini tutafanya vizuri hapa Uganda.”
Katika hatua nyingine Mexime amesema Benchi la Ufundi la Taifa Stars limekaa chini na Wachezaji wote na kuzungumza nao mambo ya kuwajengea ujasiri wa kupambana bila kuchoka, huku wakiwataka kusahau yaliyopita katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Amesema mbali na kuwatengeneza katika mtazamo huo, pia wamewaandaa kisaikolojia wachezaji wote na sasa wanasubiri kesho ifike, ili waingie Uwanjani kupambana.
“Tumekaa chini na wachezaji wetu wote, tumewajenga kisaikolojia kuhakikisha wanapambana katika mchezo wa kesho na kupata ushindi, ninaamini tutapata ushindi na kurudisha heshima katika taifa letu In Shaa Allah.” amesema Mexime ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa Taifa Stars
Kikosi cha Taifa Stars kiliondoka Dar es salaam jana jioni kuelekea Kampala-Uganda, tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa kwenye Uwanja St Marry’s.
Taifa Stars itatakiwa kusaka ushindi wa zaidi ya bao moja dhidi ya Uganda, ili kukata tiketi ya kushiriki Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ zitakazounguruma nchini Algeria mwaka 2023.