Klabu ya Singida Big Stars imeachana na aliyekuwa winga wake mshambuliaji, Harrison Mwendwa ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu iingie nae mkataba wa mwaka mmoja.
Nyota huyo aliyesajiliwa kutoka Kabwe Warriors ya Zambia ili kuongeza nguvu eneo hilo ameachwa rasmi huku ikielezwa sababu kubwa ni majeruhi.
Akizungumza kutoka Mwanza, Kocha Msaidizi wa Singida, Mathias Lule alisema wameamua kuachana na nyota huyo kwa makubaliano ya pande zote mbili.
“Ni kweli tulimpa mkataba ila baada ya kutoridhishwa na kiwango chake tumeamua kuachana naye, tuligundua timu aliyotoka alikaa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha na alipofika hapa alishindwa kuendana na kasi ya wenzake,” alisema Lule.
Mkurugenzi wa Masoko na Fedha wa klabu hiyo, Muhibu Kanu alisema wanatambua ubora wa nyota huyo, ingawa wao kama viongozi hawakuwa tayari kumvumilia ndio maana baada ya kuondoka kwake wakamsajili Muargentina, Miguel Escobar.
Hii ni mara ya pili kwa Mwenda kufeli kucheza soka la Tanzania baada ya awali kutua kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Simba, hata hivyo dili hilo lilishindwa kufikiwa kwa kile kilichoelezwa kushindwa kufikia muafaka wa pande mbili.