Zimebaki siku mbili Azam FC iingie uwanjani kucheza mechi ya mzunguko wa tatu wa Ligi Kuu Bara dhidi ya mabingwa watetezi Yanga huku kipa mpya wa timu hiyo Ali Ahmada akifunguka kuitamani mechi hiyo ili aonesheshe makali yake.
Ahmada mwenye uraia pacha wa Ufaransa na Comoro akiwa na wasifu mkubwa wa kucheza timu mbalimbali barani ulaya ikiwemo timu ya taifa ya Ufaransa kwa vijana (U-21) mwaka 2011 kabla hajabadili mawazo na kuanza kuidakika Comoro amesema haiogopi Yanga lakini anaiheshimu na anatamani kucheza nao ili amalizane naoi mapema na kuendelea na mechi nyingine.
“Yanga ni timu ngumu lakini sinahaja ya kuiogopa kwani tupo kwenye ligi moja na wote tunawania ubingwa, zaidi nahitaji kucheza dhidi yao kwani hata sisi (Azam) tunaendelea kujiandaa vizuri kuwakabili,”alisema Ahmada mwenye umbo na kimo kirefu na kuongeza;
“Kwa uzoefu wangu nafurahi kuwa hapa kwani ni timu yenye kila kitu muhimu pia inawachezaji wengi wa kimataifa hakuna tofauti kubwa na timu nilizotoka hivyo hakuna mechi naiogopa bali zote nazichukulia kwa uzito sawa na nipo tayari kucheza na kila timu.”
Kipa huyo pia alieleza msimu huu kuwa wakwaza kwake kucheza Ligi za Afrika na ameshangaa kuiona Tanzania ikiwa na mashabiki wengi wanaopenda mpira na kuonyesha mapenzi kwa timu zao.
“Nilishangaa nilipokuja hapa Afrika kwa mara ya kwanza ndani ya Azam na kukuta timu ikiwa imeimarika. “Watu wa hapa wanapenda sana soka na wanaonesha upendo mkubwa kwa timu na wachezaji wao jambo ambalo sikutarajia hapo awali na kwa sasa najiona mwenye deni juu ya mashabiki wa Azam na Ligi Kuu kwa ujumla,” alisema.
Kwa upande wake, kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Mhispania Dani Cadena ameweka wazi kuendelea kukinoa kikosi hicho kwa ajili ya mechi ijayo na Yanga.
“Tunaendelea kujiandaa kwaajili ya mechi hiyo na kufika siku ya mchezo naamini tutakuwa tayari kuingia uwanjani kupambania matokeo chanya,” alisema Cadena aliyepokmea mikoba ya Mmarekani Abdihimid Moallin aliyepangiwa majukumu mengine ndani ya Azam.