KOCHA wa Yanga, Nassredine Nabi amemwangalia Bernard Morrison ‘BM33’ na kusema huyu wa sasa ndiye anayemjua kutokana na kurejea kwenye kiwango chake tofauti na alivyojiunga kwenye maandalizi ya msimu mpya alipokuwa hana utimamu wa kimwili.
Nabi alisema, wiki kadhaa nyuma Morrison alionekana kuwa hovyo licha ya kumwandalia programu maalumu ya kujiweka fiti, lakini kwa sasa anavyomwona mazoezini na hata kwenye mechi za kirafiki anaonekana ameiva tayari kuleta balaa uwanjani dhidi ya wapinzani wa Yanga.
Kocha huyo alisema baada ya kuona Morrison hawa kiwango alichokitaka, alimpangia programu maalumu ya kufanya mazoezi ya nguvu akiwa chini ya Kocha wa Viungo, Helmy Gueldich ambayo sasa imeonekana kuwa na faida kwake.
“Alivyo Morrison wakati huu ni tofauti na awali alipojiunga na kikosi, programu maalumu ya mazoezi imemsaidia na kuongeza utimamu wa mwili wake katika kushindana ingawa hajafika pale ninapohitaji kumwona,” alisema Nabi na kuongeza;
“Naamini Morrison akiwa fiti asilimia kubwa, kwanza atacheza mechi mfululizo akiwa katika kiwango cha juu tofauti na michezo mitatu ya kimashindano aliyocheza hadi sasa ndani ya kikosi chetu.”
“Miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri katika kikosi chetu kwa sasa Morrison ni mmoja wapo amefunga bao moja na kutoa pasi ya mwisho moja, amehusika kwenye mabao mawili muhimu yaliyochangia kutupa pointi sita Ligi Kuu tena michezo migumu ya ugenini.
“Kama akifika katika utimamu wa mwili na kuwa fiti kama ninavyohitaji kutoka kwake, atakuwa kwenye kiwango bora zaidi ya misimu yote mitatu aliyocheza soka hapa nchini.”
Nabi pia alisema Morrison ana uwezo wa kutengeneza nafasi za kufunga na muda mwingine kufanga mabao aina mbalimbali na uwepo wake uwanjani muda mwingi unawapa wakati mgumu wapinzani.
Nabi alisema ikitokea kuna nafasi nyingine mashindano kusimama kama ilivyo kwenye wiki mbili hizi atakuwa anatengeneza ratiba nyingine ya kumwandaa Morrison kama ilivyofanya katika wakati huu.
“Tunahitaji kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa na yale ya ndani uwezo wa wachezaji kama Morrison tena akiwa fiti itakuwa na faida kwetu kufikia malengo hayo tuliyojipangia,” alisema.