Mshambuliaji wa Paris Saint-Germain na timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe amesema anamheshimu sana mchezaji mwenzake Neymar lakini uhusiano wao umekuwa na pande mbili kuna muda wanakuwa na uhusiaono mzuri na kuna muda wanakuwa na migogoro.
“Huu ni mwaka wa sita na Neymar. Daima tumekuwa na uhusiano kama huu, kwa msingi wa heshima, lakini wakati mwingine na wakati wa joto na baridi” alisema Mbappe.
Uhusiano wa Mbappe na nyota huyo wa Brazil unafahamika kuwa haukuwa mzuri tangu Lionel Messi alipowasili Paris mwaka jana.
Wawili hao walizozana uwanjani katika mechi ya PSG dhidi ya Montpellier mapema msimu huu huku Neymar akikataa kumruhusu Mbappe kupiga mkwaju wa penati, Mfaransa huyo tayari alikuwa amekosa penati moja mapema kwenye mchezo huo, lakini Neymar alifunga penati hiyo katika ushindi wa 5-2.
”Unapokuwa na wachezaji wawili wakubwa, unakuwa na wakati kama huo, lakini kila mara kwa heshima na kwa maslahi ya PSG” alisema Mbappe.
PSG kwa sasa wako kileleni mwa ligi kuu nchini Ufaransa baada ya kuangusha pointi mbili pekee katika michezo sita. Watacheza tena leo dhidi ya Juventus kwenye Ligi ya Mabingwa.