Achana na umaarufu wa Karim ‘Mandonga’ Said, unaambiwa mapambano yote aliyocheza hivi karibuni, ni ya maonyesho ambayo hayajampa rekodi yeyote kwenye renki.
Pambano lake la Machi 26 alilochapwa kwa Knock Out (KO) na Magambo Christopher ndilo lilikuwa la mwisho kuingizwa kwenye rekodi, huku lile la Shaban Kaoneka na mengine yaliyofuatia yakiwa ya maonyesho ambayo hayatambuliki kwenye rekodi zake za ngumi.
Baada a kupigwa na Kaoneka, Mandonga alizichapa jijini Dar es Salaam kwenye viwanja vya Leaders, kisha Kigoma ambako kote alishinda, lakini matokeo ya mapambano hayo yaliishia ulingoni.
“Sijui ni kwanini mapambano yangu hayaingizwi kwenye rekodi, nimeshalalamikia sana juu ya hilo, hadi kwenye Kamisheni (TPBRC) lakini naona hakuna kinachofanyika,” amesema.
Kwa mujibu wa mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec), Mandonga amepigana mapambano matano, amepigwa mara 3 zote kwa KO, ametoka sare mara moja na kushinda moja tangu 2015.
Rais wa TPBRC, Chaurembo Palasa amesema mapambano ya karibuni ya Mandonga yalikuwa ya maonyesho na si kumpa rekodi yoyote kwenye ngumi.
Alisema rekodi za mapambano ya karibuni ya Mandonga anayekamata nafasi ya 22 kati ya mabondia 32 nchini na wa 1,171 kati ya 1,513 duniani kwenye uzani wa middle hazijaingizwa huko kwa kuwa ni mapambano ya maonyesho.
“Kuanzia lile la Kaoneka, hadi lile alikwenda kupigana Kigoma yote hayakuwa mapambano rasmi, bondia anaposaini mkataba kuzichapa kuna kuwa na makubaliano, hivyo mapambano yake kutoingizwa pia ni makubaliano.
“Ni kama Mayweather ‘Floyd aliwahi kuwa bondia namba moja duniani kwenye uzani wa welter’ kuna mapambano anapigana ya maonyesho tu, hayatambuliki kwenye renki, ndivyo ilivyokuwa hata kwa Mandonga.
“Pambano lake la Mtwara (la Septemba 24) na lile la Morogoro (la Novemba atazichapa na Said Mbelwa), hayo sasa ndiyo yatakuwa rasmi na yataingizwa kwenye rekodi za Boxrec,” amesema.