Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Jumamosi Septemba 17 itaingia kambini kwa maandalizi ya mechi tatu za kirafiki kimataifa dhidi ya Libya na Uganda.
Mechi hizo zote zitachezwa Libya ambako Taifa Stars na Uganda zimepata mwaliko mwalumu ikiwa ni maandalizi ya mechi zijazo za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (AFCON).
Baada ya kuanza kambi Dar es salaam itakayodumu kwa siku chache, Taifa Stars itasafiri kwenda Libya na mechi ya kwanza katika mechi hizoo itakuwa Libya dhidi ya Uganda Septemba 21, 2022.
Tanzania itajitupa uwanjani Septemba 24, 2022 kucheza na Uganda na mechi ya mwisho itacheza na Libya Septemba 27 kisha kurudi Tanzania.
Michezo hiyo iliyo kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) zitakuwa na faida kwa makocha wa timu zote kimbinu na mipango hususani Taifa Stars na Uganda ambazo hapo baadae zitakutana kwenye mechi za kuwania kufuzu Afcon.
Ikumbukwe siku chache zilizopita, Taifa Stars ilishindwa kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) kwa kutolewa na Uganda kwa jumla ya mabao 4-0 baada ya kufungwa 1-0 nyumbani na kuchapwa 3-0 ugenini.