Nahodha Msaidizi na Beki wa Kushoto wa Simba SC Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ amefunguka kwa mara ya kwanza kuelekea mchezo wa ‘Kariakoo Derby’ unaosubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki wa soka nchini Tanzania.
Simba SC itaalikwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Jumapili (Oktoba 23), kucheza dhidi ya Young Africans itakayokuwa mwenyeji wa mchezo huo, uliopangwa kuanza mishale ya saa Kumi na Moja jioni kwa Saa za Afrika Mashariki.
‘Tshabalala’ amesema wanakwendea katika mchezo huo wakiwa na Deni kubwa kwa Mashabiki na Wanachama wa Simba SC, baada ya kushindwa kuwafurahisha kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii uliopigwa Agosti 13, ambapo Young Africans ilichomoza na ushindi wa 2-1.
Amesema wanajua Deni hilo halina njia ya mkato zaidi ya kulipwa katika mchezo wa Jumapili (Oktoba 23), na ndio maana wamejiandaa kikamilifu kwa kufanya mazoezi makali, ili kutimiza wajibu wa kushinda na kupata alama tatu muhimu.
“Huku kwetu wachezaji kama tuna deni vile, kila mmoja kwa nafasi yake atakwenda kupambana kuliko kawaida na wale ambao watakuwa wanaangalia mchezo watashangaa, tunafanya hivyo kwa sababu tunahitaji ushindi,”
“Ushindi utakuwa na maana kubwa kwetu tutajiweka kwenye mazingira mazuri katika msimamo wa Ligi Kuu na utakuwa mwendelezo wa kufanya vizuri kwa siku za hivi karibuni.”
“Hatuna matokeo mazuri dhidi ya Young Africans, hivi karibuni wametufunga mara mbili mfululizo, lakini kwa maandalizi tulioyafanya kila kitu kinakwenda vizuri naamini tutapata matokeo bora kwenye mchezo wa Jumapili.” amesema Tshabalala
Simba SC na Young Africans zinakwenda kukutana Jumapili (Oktoba 23) zikiwa zimejikusanyia alama 13 kila mmoja, baada ya kucheza michezo mitano msimu huu 2022/23.