Home Habari za michezo WAARABU 6 WAIMEZEA MATE SIMBA CAF…WAKIKOSWA KOSWA SANA..WATAPANGWA NA HAWA…

WAARABU 6 WAIMEZEA MATE SIMBA CAF…WAKIKOSWA KOSWA SANA..WATAPANGWA NA HAWA…

KWA mara nyingine Simba imeendelea kuwa na rekodi nzuri kimataifa. Ndiyo klabu pekee ya Tanzania iliyofuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayoanza Februari mwaka lakini droo itachezeshwa mapema mwezi ujao.

Simba iko chungu namba tatu na timu za CR Belouizdad na JS Kabliye kutoka Algeria na Al Hilal ya Sudan ambayo bado inakumbukwa kwani iliinyima Yanga Yanga nafasi ya kwenda makundi.

Timu ambazo zipo chungu kimoja haziwezi kukutana kwenye makundi hivyo Simba inaweza kupangwa wababe sita wa Uarabuni ambao ni El Merikh, Al Ahly, Wydad Athletic, Esperance, Raja Casablanca, Zamalek. Nyingine ni Horoya AC, Petro Atletico, Cotton Sport, Vipers, AS Vita na Mamelod Sundowns.

Chini ya wazawa Juma Mgunda akisaidiana na Selemani Matola wanakabiliwa na mtihani mzito wa kufanya makubwa kwenye hatua hiyo ya makundi ambayo lengo mama ni kutinga nusufainali, mfupa uliowashinda makocha waliowatangulia wengi wao wakiwa raia wa kigeni.

AL AHLY
Imekuwa na mafanikio makubwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika ikitwaa mara 10 na sio wageni wa Simba kwani mara ya mwisho zilikutana msimu wa 2020/21 zilipokuwa kundi A ambalo Simba iliibuka kinara na pointi 13 nyuma yao iliyoshika ya pili na 11.

Licha ya kukutana mara kadhaa na ubora ilionao ila Al Ahly imekuwa ikifungwa na Simba katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwani mara yao ya mwisho ilikuwa Februari 23, 2021 ilipolala bao 1-0 lililofungwa na Luis Miquissone.

COTON SPORT
Ni WaCameroon wana rekodi zuri kwenye michuano ya kimataifa kwani wamefika fainali ya Kombe la CAF 2003 na Ligi ya Mabingwa Afrika 2008 pia wakifika nusu fainali 2013.

AL MERRIKH
Ni Wasudan hawa. Wamewahi kukutana na Simba kundi moja la A msimu wa 2021/22 lililokuwa na Al Ahly, AS Vita Club na kumaliza mkiani na pointi mbili.

AS VITA CLUB
Sio wageni kwa Simba kwani mara ya mwisho kukutana ulikuwa msimu wa 2021/22 walipopangwa kundi A kwenye Ligi ya Mabingwa ambapo ilipoteza mechi zote mbili ikianza na kichapo cha 1-0 Februari 12, 2021 kisha 4-1, Aprili 3, 2021 na kuifanya timu hiyo ya Kinshasa kumaliza ya tatu na pointi saba.

VIPERS
Vipers walifanya maajabu kwa kuitoa TP Mazembe na kutinga hatua ya makundi kwa mara ya kwanza kwenye historia ikiwa ni timu ya kwanza kufanya hivyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika kutoka nchini Uganda tangu KCCA ilipoingia mwaka 2018.

WYDAD CASABLANCA
Wawakilishi hawa wa Morocco ndio ambao wanashikilia taji la Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya msimu uliopita kuwafunga mabingwa watetezi – Al Ahly ya Misri kwa mabao 2-0 na kufikisha ubingwa wa tatu wa mashindano hayo baada ya awali kuchukua mwaka 1992 na 2017.

ESPERANCE
Msimu uliopita timu hii kutoka Tunisia iliishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku ikiwahi kutwaa ubingwa huo mara nne (1994, 2011, 2018 na 2019).

RAJA CASABLANCA
Ina ubingwa wa tatu kwenye Kombe la Afrika pia ikiwa ni timu ya pili Afrika na ya kwanza kutoka Uarabuni kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa Klabu zilizofanyika Morocco mwaka 2013 ambapo ilifungwa mabao 2-0 na Bayern Munich ya Ujerumani.

MAMELODI SUNDOWNS
Timu hii kutoka Pretoria, Afrika Kusini imewahi kutwaa ubingwa wa Afrika 2016 ikishikilia rekodi ya ushindi mkubwa ilipoifunga Cote d’Or ya Shelisheli mabao 11–1 ikiwa nyumbani na 16-1 kwa ujumla katika raundi ya kwanza msimu wa 2019/20.

ZAMALEK
Ni miongoni mwa timu za Misri zilizofanikiwa zaidi ikitwaa ubingwa wa Afrika mara tano kuanzia (1984, 1986, 1993, 1996 na 2002).

HOROYA AC
Iko katikati mwa mji mkuu wa Guinea, Conakry ambapo mafanikio yake makubwa kwenye Ligi ya Mabingwa ni kufika robo fainali msimu wa 2018/2019.

PETRO ATLETICO
Miamba hii kutoka Angola inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya saba ambapo msimu uliopita ilifanya vizuri na kuishia hatua ya nusu fainali.

MSIKIE MGUNDA
Baada ya kuifikisha timu hiyo hatua ya makundi kaimu kocha Juma Mgunda alikaririwa akisema michuano ya kimataifa njia pekee ya kufanya vizuri ni kutumia vyema uwanja wa nyumbani pamoja na kuwaandaa wachezaji kimwili na kiakili.

“Siri kubwa ni umoja kuanzia kwa wachezaji wenyewe, benchi la ufundi na viongozi wetu ambao kwa pamoja walikuwa nasi bega kwa bega,” anasema Mgunda.

MAKOCHA WAWILI
Msimu huu tayari imenolewa na makocha wawili ikianza na Mserbia Zoran Maki aliyechukua nafasi ya Mhispania Pablo Franco na Juma Mgunda aliyejiunga na kikosi hicho Septemba 7 akitokea Coastal Union.

Akiwa na kikosi hicho, Zoran alikiongoza katika michezo miwili ya Ligi Kuu Bara na kukiwezesha kushinda yote akianza na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Geita Gold, kisha 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Baada ya hapo Mgunda akaanza rasmi kibarua cha kuifundisha katika michezo iliyofuata akianza na ile la kimataifa.
Alianza na ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo wa hatua ya awali dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi ugenini Septemba 10 kisha kuifunga 2-0 Septemba 18 na kukutana na Primeiro de Agosto ya Angola kwenye hatua ya mwisho kusaka nafasi ya makundi.

Mchezo wa kwanza uliopigwa Angola Oktoba 9, Simba ilishinda mabao 3-1 kisha kushinda tena 1-0, Oktoba 16 na kumfanya Mgunda kuivusha hatua ya makundi akiwa ni mzawa wa pili baada ya Tito Mwaluvanda kufanya hivyo akiwa na Yanga 1998.

KIKOSI KAZI
Mchezaji tishio ni Mzambia Moses Phiri ambaye kwenye Ligi ya Mabingwa pekee amefunga mabao matano huku Ligi Kuu Bara akifunga manne akipitwa moja tu na Reliants Lusajo wa Namungo mwenye matano.

Simba inaundwa na mastaa 28 ambao ni, Aishi Manula, Beno Kakolanya, Ferouz Ahmed, Ally Salim, Israel Mwenda, Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Nassoro Kapama, Erasto Nyoni na Kennedy Juma.

Wengine ni, Joash Onyango, Mohamed Quattara, Henock Inonga, Mzamiru Yassin, Victor Akpan, Jonas Mkude, Sadio Kanoute, Peter Banda, Jimmyson Mwanuke, Clatous Chama, Pape Ousmane Sakho, Nelson Okwa, Augustine Okrah, Kibu Denis, Moses Phiri, John Bocco na Habibu Kyombo.

SOMA NA HII  GOMES WA SIMBA AWEKA REKODI YAKE DAKIKA 360

1 COMMENT