Home Habari za michezo EXCLUSIVE: KAGERE AANIKA A-Z ALIVYOFANYIWA NA SVEN NA KILICHOMTOKEA MPAKA SIMBA WAKAMUACHA…

EXCLUSIVE: KAGERE AANIKA A-Z ALIVYOFANYIWA NA SVEN NA KILICHOMTOKEA MPAKA SIMBA WAKAMUACHA…

Akiwa kwenye maandalizi ya msimu mpya nchini Misri na kikosi cha Simba, ghafla mshambuliji, Meddie Kagere alirejea nchini, wakati mashabiki wakijiuliza kulikoni?, akaibuka kwenye kikosi cha Singida Big Stars ambacho anakitumikia msimu huu.

“Ilikuwa lazima iwe hivyo, japo viongozi wengi hawakupenda niondoke, lakini sikutaka mimi niwe ni sababu,” anasema Kagere katika mahojiano maalumu na gazeti la Mwanaspoti.

Kagere ambaye alicheza Simba kwa misimu minne akichukua tuzo ya mfungaji bora mara mbili sanjari na ubingwa, anasema kocha Zoran Maki alionyesha dalili za kutomhitaji mara tu baada ya kuajiriwa na timu hiyo.

“Wengi hawakufahamu ni kwa nini niliondoka Simba, japo waliniona kwenye maandalizi ya msimu nikiwa kule Misri na walifahamu kuwa niko kwenye timu kwa msimu mwingine zaidi japo kocha hakunitaka.

“Ambacho nilikuwa nakifahamu ni kwamba natakiwa kufanya kazi ambayo timu inahitaji, nilifanya hivyo siku zote nikiwa Simba, japo kuna changamoto nilipitia na alipowasili Zoran naye alitaka kuwaleta wachezaji.

“Alisema anataka washambuliaji wawili, viungo wawili na beki, nikajiuliza inawezekana vipi timu kuwa na washambuliaji wanne wa kigeni? kichwani mwangu nikajiongeza kwamba hiyo ni dalili wananiambia tafuta timu nyingine hutakiwi,” anasema.

“Viongozi waliongea, lakini msimamo wa kocha ulikuwa ni huo, sikujali kwa kuwa nilikuwa Simba kama sehemu ya familia, niliona ni wakati wangu wa kuondoka japo viongozi hawakutaka niondoke, lakini hawakuwa na namna nyingine kwa kuwa kocha tayari kasema na klabu inamhitaji kocha.

“Kama wangeng’ang’ania nibaki, timu isipofanikiwa watasemaje? wakati mimi sikuwa chaguo la kocha, waliniambia wanipeleke timu nyingine kwa mkopo.

“Kwa mchezaji hakuna kitu kibaya kama hicho, inaonekana ni kama kiwango chako kimeshuka, kwangu mimi haikuwa hivyo, niliwambia kuliko kunitoa kwa mkopo ni bora waniache niondoke.”

“Sikuwa na tatizo kabisa, niliondoka Simba vizuri na hata waliponiomba kwenye Simba day niwepo, nilifanya hivyo ingawa wakati huo tayari nilishasaini mkataba na Sigida.”

“Kikubwa ni umeondoka kwenye timu na kuacha historia gani? sikuacha historia mbaya Simba, najivunia katika misimu minne nimekuwa mfungaji bora mara mbili, nimeishi vizuri na kila mchezaji, viongozi na hata mashabiki, hiki ni kitu ambacho najivunia,” anasema.

KUTOANZA SINGIDA

“Hapa kila mchezaji anataka kucheza, nafasi ya kucheza ipo, lakini lazima upambane haswa, mimi sikuwa na Singida kwenye pre season, nilikuwa Simba, wachezaji waliopo walikuwa pamoja na wanaelewana.

“Kuingia kwangu kwa kiasi fulani kuliwapa ugumu wacheze vipi na mimi, hawafahamu mijongeo yangu, hivyo ilikuwa changamoto na mimi kupata ugumu wa kuwa kwenye kikosi cha kwanza, hata nilipoingia bado ilikuwa ngumu, lakini polepole tumeanza kuelewa,” anasema.

Kabla ya kutua Singida, Kagere anasema alipata ofa Arabuni; “Niliona Arabuni kwanza ni mbali na nyumbani, halafu ofa yao si zuri, mtu ambaye yuko Dar es Salaam anakuzidi, hivyo kwanini niende? ili kupata sifa kwamba niko Arabuni halafu nalipwa kiduchu?.

“Kabla ya kwenda Singida niliwaza kurudi Rwanda nitulie kidogo, lakini nikajiambia mbona uwezo wa kucheza nje bado ninao na tangu 2012 nilivyotoka nyumbani sikuwahi kurudi kucheza huko, nikasema wacha nijiunge na Singida ambao walinipa kile nilichokitaka.

“Singida na Dar es Salaam kuna tofauti, Dar ni jiji, lakini mimi uwa sina mambo mengi, hivyo sikuona shida kuishi Singida kwa sababu ya mpira, ninachokifanya ni kazi tu,” anasema.

SHIDA ILIANZIA KWA SVEN

“Mchezaji ni fitiness, unapopata nafasi ya kucheza mara kwa mara unazidi kuwa fiti, lakini baadae kocha aliamua kutonicheza kwa sababu zake binafsi.

“Mimi si muongeaji, naamini kila kitu kina sababu na hakiwezi kuwa na mwisho, katika soka kocha ni mtu ambaye anaweza kumfanya mchezaji kuwa kwenye ubora wa hali ya juu, lakini pia huyo huyo akakuporomosha kiwango.

“Nakumbuka kuna kipindi kocha anakuonyesha dhahiri hakutaki, au anakuchukia sababu tu wewe mchezaji ni staa.

“Sven aliniambia kwenye timu yake hapendi mastaa, nilimwambia hiki kinachotokea sio mimi nataka ila ni mashabiki ndiyo wanafanya hivyo sababu wanaridhishwa na kazi yangu,” anasema.

“Watu walikuwa wakiniona, nikipewa nafasi hata kama ni dakika 10, naenda kufanya kazi, kwani niliamini sichezi kwa sababu ya kocha apate matokeo, la hasha bali nikifanya vizuri ndipo natengeneza jina langu zaidi, hivyo nikipewa nafasi hata kama ni dakika mbili nitapambana kadri ya uwezo wangu,” anasema.

Anasema bifu lake na Sven lilianzia kwenye timu ya taifa ya Rwanda, ambako aliomba kazi.

“Shirikisho waliniuliza kuhusu yeye, niliwaambia ni kocha mzuri, anajua kufundisha lakini ana changamoto zake, akisema ni hivi basi ni hivyo hivyo hata kama anakosea.

“Niliwaeleza ukweli wa jinsi alivyo Simba, anabishana na kila mtu ila wakimuweza kwenye tabia zake basi ni kocha mzuri, alifahamu hilo na akaja kuniambia kwamba nimemchongea, kuanzia pale tukawa tupo tofauti.”

Anasema alipokuja Gomes, yeye Kagere alikuwa akifahamiana nae kabla kwani aliwahi kumfundisha Rwanda.

“Pia naye aliwahi kuomba kazi Shirikisho, aliniambia nimuunganishie kwa kuwa kwa kiasi fulani wananisikiliza na yeye Gomes anafahamu hilo.

“Nilipowaeleza wakaniuliza kwanini ananiweka benchi, nikawaambia pia amefuata mfumo wa Sven, kwani alikuta nawekwa benchi na yeye akapita humo humo, nilikuwa na mabao 11, nikawa benchi hadi Bocco na Mugalu wakanipita.

“Siku moja wakala wa Gomes akanifuata kwa ajili ya ishu ya kupata kazi timu ya Rwanda, nikamwambia mimi sina uwezo, Shirikisho wakiridhika naye watamuajiri, lakini mimi siamui hilo, kuanzia hapo akaanza kunichukia tu.

“Kuna siku aliniambia mimi ndiyo kocha, hivyo tutaona kama utacheza, labda Bocco na Mugalu wawe hawawezi hata kutembea, lakini kama wanatembea nitawapanga hata kama wanaumwa basi wakasimame tu.”

Anasema aliongeza mkataba mpya wa miaka miwili Simba bila kocha kufahamu.

“Tulikwenda pre season Morocco, niliporudi kujiunga na timu akaniuliza, wewe umerudi kufanya nini? akaambiwa nimeongeza mkataba wa miaka miwili, chuki ndipo ikaongezeka.”

Anasema msimu huo walicheza na Yanga, Simba ilifungwa, kocha hakumpanga kwenye kikosi chake, akalazimika kuondoka kurudi nyumbani.

“Tulikuwa kambini, alipotaja kikosi mimi sikuwemo, nikamwambia kocha mbona unaniacha wakati hizi ndizo mechi zangu, hakunijibu nikawaaga wenzangu na kuwatakia mechi njema nikarudi nyumbani,” anasema.

Kagere anasema Simba ilikwenda kucheza Afrika Kusini, walizungumza wachezaji na kukubaliana ile mechi wacheze wapambanaji, sio wapiga pasi.

“Tulikubaliana hivyo, nahodha akaenda kumwambia, lakini hakukubali, hakukaa muda mrefu naye akaondolewa,”.

MFALME WA DABI

“Kuna mechi kipa ananitukana ili anitoe mchezo, lakini wala sikuwahi kupaniki, niliamini ukijiamini unafanikiwa.

“Nikiwa Kenya, nilipewa jina la king of dabi ‘mfalme wa dabi’ hapa Tanzania Simba na Yanga ni dabi lakini ina amani, nakumbuka nikiwa Gor Mahia, dabi yao na AFC Leopards ilikuwa ni vita.

“Kuna siku mechi ilisimama, kisa tu niliambiwa siku hiyo sifungi, nilipewa pasi nzuri ya goli, naenda kufunga beki akaona isiwe tabu kwa kuwa walishaniapia siku hiyo sifungi, akazuia mpira kwa mkono, ikawa penalti.

“Mpigaji nilikuwa mimi, baadhi ya mashabiki walinigomea, wakasema penalti haipigwi, bora apige mwingine lakini sio mimi sababu niliambiwa siku hiyo sifungi, sijui ilikuaje nikamwagiwa majivu usoni, vurugu zikaanza, hapa Tanzania dabi zina amani.”

Anasema soka la Kenya wanatumia nguvu, lakini pia kuna matukio ya kukutoa mchezoni.

“Yote hayakunivuruga, kuna muda beki anakupiga ngumi makusudi, unatemewa mate, unatukanwa, unachezewa faulo ila nilikuwa kimya tu nacheza, lakini nifanyie yote kabla sijafunga, nikifunga ndipo malipo yangu utayaona, nitakupeleka nitakavyo uwanjani hadi ukasirike,” anasema.

“Mimi nakumbuka kuna timu ilikuwa rangi nyekundu ni mwiko, nilikuwa na mpira wangu wa rangi hiyo, mashabiki waliutoboa toboa nakuninunulia wa rangi nyingine, kule hadi jezi wanakuvua.

“Kuna mchezaji alikuwa na Range nyekundu, mashabiki walimnyang’anya wakaenda kuibadili rangi, kwenye dabi wakianza kupigana hadi Polisi wanawashindwa. Anasema kuna timu alikwenda kucheza Lebanon, ambayo ilikuwa inapambana isishuke.

“Walinipa mkataba wa miezi sita, wakasema hawana pesa ya usajili lakini tulikubaliana wanipe mshahara mzuri, wakaniambia pia kila goli nitakalofunga watanipa dola 200, nikitoa pasi ya goli dola 100 achilia mbali bonasi ya timu.

“Lakini ilikuwa kwenye nchi ambayo milio ya mabomu ilikuwa nje nje, mko mazoezi mnasikia tayari kimenuka, bomu linapigwa uwanja wote unatetemeshwa, wakati mwingine hadi moshi mnauona, wakati mwingine mmelala mnaamshwa mshuke chini hali si shwari.

“Kuna Mbrazil alikuwa rafiki yangu alitoroka kurudi kwao, siku amefika tuko uwanjani tunafanya mazoezi, lilipigwa bomu nyuma tu ya uwanja, kwa kuwa sisi tumeshazoea tuliona kawaida, yeye akauliza, mmesikia hicho kilichopiga? tukamwambia tumezoea.

“Siku hiyo usiku aliniambia yeye hawezi anaondoka, lakini niliyavumilia katika upambanaji na utafutaji maisha,” anasema.

ATUE YANGA

“Nikiwa Kenya, Yanga walinifuata, ilikuwa ni kipindi cha Manji (Yusuf), ni kati ya 2013 au 2012, nilikuja hadi Tanzania, tukafanya mazungumzo, lakini wakati huo pia ndipo Bidvest ya Afrika Kusini wakawa wananihitaji, Yanga wakaniambia niende nikishindwana nao nirudi.

“Nilivutiwa kucheza Afrika Kusini, nilikwenda lakini tofauti na matarajio kwamba nikifika kule baada ya vipimo wananisajili wakataka kwanza kunifanyia majaribio, sikuweza utaratibu huo ndipo wakala wangu akanipeleka Esperance ya Tunisia, nilifanya vipimo wakanipa mkataba, hiyo ndiyo ikawa sababu ya kutocheza Yanga,”.

Anasema baadae alikwenda Lebanon, akarudi Rwanda, akaenda Ulaya kisha Kenya ambako Singida na Simba walimtaka na Yanga pia ilimfuata kwa mara nyingine.

“Sikuwa nayafahamu mazingira ya soka la Tanzania, ikabidi niulize, kilichonivutia kwa Simba ilikuwa ikicheza Ligi ya Mabingwa, nikajiunga nao, tangu 2013 msimu huu ndio wa kwanza sijacheza Ligi ya Mabingwa, huko kote nilikokuwa nimecheza,” anasema.

KURUDI SIMBA, YANGA

“Mchezaji unapaswa kupata muda wa kucheza tu, mimi misimu miwili ya kwanza Simba nilipata nafasi hiyo ndiyo sababu nilikuwa mfungaji bora.

“Natamani kuwa mfungaji bora, ingawa msimu huu ni mgumu na dalili zinaoneka mapema, kwa kuthibitisha hilo, muangalie mfungaji bora wa msimu uliopita sasa anapambana.

“Hii ndio maana ya Ligi ngumu, timu zaidi ya mbili zikiwa na uwezo kipesa inatoa ushindani zaidi, hivi sasa ukiachana na Simba, Yanga na Azam timu nyingine ndogo pia zimenyanyuka kipesa ikiwamo Singida.

MECHI ANAYOIKUMBUKA

“Nafikiri tulicheza na Tanzania Prisons, ni mechi ambayo nilifunga bao, ulikuwa ni mwanzo mzuri kwangu na tangu hiyo siku kwenye mechi zote za Ligi za kwanza nilikuwa nafungua milango ya mabao.

“Siku zote mechi ya kwanza inakupa maono mazuri, tulishinda bao 1-0, goli nikifunga mimi, kipindi ambacho tulitoka kucheza Ngao ya Jamii na Mtibwa Sugar, wakati huo nilikuwa nikisikia mashabiki wakihoji mbona sifungi, baada ya kucheza mechi kadhaa za kirafiki.”

KUIFUNGA YANGA

“Kucheza timu kubwa ni rahisi kuliko ndogo sababu wote mnakuwa ni maproo na mnajua, hivyo ni kuwa makini tu sababu mpira ni kawaida, nilikuwa nawambia wenzangu nikianza mechi ya Azam lazima nifunge.”

“Tunatakiwa kuwekeza ili utakapostaafu watu waendelee kukufahamu kuwa ulikuwa mchezaji, maisha ya ustaa ukiwa mchezaji ni mafupi, utaimbwa, sehemu zote za starehe utakuwepo, lakini bila kuwekeza kipaji chako hakitakuwa na maana baada ya kustaafu.

“Nidhamu kwenye kila kitu inahitajika, mimi leo kuna mawakala wananiambia niwatafutie washambuliaji kama mimi, kuna wakati naweza nikawapeleka wachezaji chipukizi sehemu, wananiambia tunavyokufahamu, huyu uliyetuletea mwambie alinde heshima yako, bunafsi ni muumini mzuri wa nidhamu.”

SOMA NA HII  KIFUNGO CHA MANARA CHAFUNGUA MIDOMO YA WADAU WA SOKA...WAIBUKA NA HOJA HIZI NZITO ZA KUSHINDILIA...