Home Habari za michezo MABEKI YANGA WAMTANGAZIA KIAMA MOSES PHIRI…WAAPA ‘KULALA NAYE MBELE’…

MABEKI YANGA WAMTANGAZIA KIAMA MOSES PHIRI…WAAPA ‘KULALA NAYE MBELE’…

Habari za Simba

Huko Yanga unaambiwa mabeki wa timu hiyo hawataki masihara kwani wameweka wazi kuwa hawatakubali kufanya makosa na kuwaruhusu washambuliaji wa Simba wakiongozwa na Moses Phiri kupata nafasi ya kuwafunga.

Simba kwa sasa wanatamba na ubora wa mshambuliaji wao Moses Phiri ambaye ameifungia timu hiyo mabao 4 katika michezo 5 ya ligi kuu msimu huu, jambo ambalo ni tishio kuelekea mchezo wa leo dhidi ya Yanga.

Akizungumza na gazeti la  Spoti Xtra, beki wa kati wa Yanga, Dickson Job, alisema kikubwa kwa upande wao kuelekea katika mchezo huo wamejipanga kuhakikisha hawaruhusu makosa kwa washambuliaji wa Simba ili wasilete madhara katika kikosi chao na kuwanyima nafasi ya kufunga.

“Lazima umakini uwepo kwetu mabeki ili tusiweze kutengeneza makosa ambayo yatasababisha kuwapa nafasi washambuliaji wa Simba kufunga.

“Mchezo huu ni muhimu kama ambavyo ipo michezo mingine, lakini kikubwa kwetu ni kupata matokeo mazuri,” alisema Job.

Naye beki wa pembeni wa Yanga, Kibwana Shomari, alisema: “Tuna kazi kubwa sisi kama mabeki kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri na haturuhusu kupitika kirahisi.

“Simba wana wachezaji wazuri, hivyo lazima tuongeze umakini na kwetu sisi tupo tayari kwa ajili ya mchezo.”

Yanga na Simba zinakutana leo Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Timu hizo msimu huu zimecheza mechi tano kila moja, zimekusanya pointi 13, Simba inaongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, Yanga inashika nafasi ya pili kwenye msimamo.

SOMA NA HII  SINGIDA BIG STAR 'WAMCHOMOA' ONYANGO MAZIMA...