Home Habari za michezo UKWELI WA STORI ZA ‘JEANS’ LA MGUNDA NA MAMBO YA KIFREEMASON…

UKWELI WA STORI ZA ‘JEANS’ LA MGUNDA NA MAMBO YA KIFREEMASON…

Kiwango cha juu kabisa cha kutomwamini Mtanzania kama anaweza kuifundisha Simba au Yanga ni hiki hapa. Juma Mgunda aliichukua Simba kama kocha. Haikueleweka kama ni kocha wa muda au wa kudumu. Mpaka sasa wengine hatujaelewa vyema.

Akaenda zake Malawi katika mechi ya kimataifa akashinda. Akarudi zake akashinda mechi za Ligi Kuu Bara kisha akawafunga tena Wamalawi. Halafu akawafunga Waangola nyumbani na ugenini. Waswahili hatukutazamia jambo hili.

Tuliamini Mgunda angechemsha mechi za kimataifa pamoja na ligi halafu atimuliwe mapema. Au tulitazamia pia kwamba Simba ingecheza vibaya halafu Mgunda angefurumushwa mapema tu. Tulipoona anasonga mbele tukaamua kutafuta jambo.

Kiwango cha juu cha kutojiamini ilikuwa ni kudai kwamba kocha wetu alikuwa habadilishi jeans yake na ndio ilikuwa siri ya mafanikio yake. kwamba Mgunda ni zaidi ya kocha. Ana mengine. Unaweza kudhani ni masihara. Kuna ambao walichukulia kama utani wa kawaida halafu kuna walioamini.

Binafsi naona ni utani wa kawaida tu lakini kinachonifumbua akili ni kwamba suala la kumhusisha tu kocha wa Kitanzania na jambo kama hili ni dharau kwa uwezo wake. Suala la kumhusisha tu na jambo hili linakupa mwanga namna tunavyowachukulia makocha wetu na wakati mwingine hata mastaa wetu.

Kwamba ukiwa Mtanzania kuna mambo fulani ya kawaida tunatazamia uyafanye, lakini kama ukizidisha zaidi ya hapo basi kuna namna ambayo inafanyika nje ya uwanja na sio kwa uwezo wako binafsi.

Kama Simba ingeajiri kocha kutoka Serbia au Ujerumani halafu ikapata matokeo kama ya Mgunda basi si ajabu tungempa majina matamu zaidi.

Tungemuita Professa, Dokta, Fundi, Genius na majina mengine. Huku kwa Mgunda tumemuita Pep Guardiola Mnene lakini hapo hapo licha ya kwamba boli linatembea, lakini bado tunahisi kuna kitu zaidi. Jeans yake.

Inanikumbusha zamani wakati Rashid Matumla alipokuwa katika ubora wake akiwadunda Wazungu pale ukumbi PTA. Kuna watu walidai kwamba Wazungu walikuwa hawamuoni Matumla ulingoni na ndio maana alikuwa anawadunda. Cha kushangaza ni kwamba kuna ngumi nyingi zilikuwa zinamuingia Matumla.

Inanikumbusha pia namna ambavyo hapa miaka ya katikati mtu alikuwa akifanikiwa sana kimaisha wanadai kwamba ni mwanachama wa Freemason. Kwamba Mbwana Samatta ni Freemason. Diamond Platnumz ni Freemason.

Kijana akipambana kusafirisha bidhaa nje ya nchi kwa juhudi kubwa na kujenga hoteli za kifahari huwa anaitwa ni Freemason. Wakati mwingine tunahitimisha mjadala wa utajiri wa mtu kwa kudai kwamba amepata mali kwa njia za kimafia.

Kwa Mgunda hesabu zilikuwa rahisi tu. Anachokifanya nakifananisha na kile ambacho kocha Eddie Howe wa Newcastle United anakifanya pale England. Mgunda alikuwa Coastal Union na alikuwa anafurahi kucheza soka la kushambulia kwa muda mwingi.

Inawezekana hili lilikuwa kosa lake katika baadhi ya mechi kubwa na ndio maana Simba na Yanga waliwahi kumuadhibu kwa mabao mengi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa sababu hakuichezesha timu yake katika nidhamu inayotakiwa.

Safari hii anafundisha timu ambayo ina wachezaji bora kuliko Coastal Union. Huenda kazi yake inakuwa rahisi zaidi kwa sababu akiwa na Coastal Union hakuwa na Clatous Chama, Augustine Okrah wala Moses Phiri. Kwanini kazi yake isiwe rahisi?

Inashangaza kwamba kazi yake inapokuwa rahisi zaidi watu wanaona hastahili, bali labda jeans yake imefanya kazi.

Yule Eddie Howe wa Newcastle United nilimuona alikuwa kocha mzuri akiwa na Bournemouth ingawa ilishuka daraja.

Timu yake ilicheza soka la kasi na la kushambulia kwa muda mwingi wa mchezo lakini haikuwa inapata matokeo mazuri kama zilivyo timu kubwa.

Kile ambacho alikuwa anakifanya na Bournemouth sasa hivi anakifanya akiwa na Newcastle United. Amepata wachezaji wenye ubora zaidi kuliko wale aliokuwa nao Bournemouth. Na sasa tunaofuatilia soka la Kiingereza tunajua kwamba Newcastle United wanaweza kwenda Top Four.

Wakati mwingine kocha anaweza kuwa mzuri lakini akaangushwa na wachezaji wake wa kawaida au sera za matajiri wa klabu kutotia pesa nyingi katika masuala ya wachezaji. Unadhani Pep Guardiola anaweza kufanya maajabu akiwa na Wolves? Haiwezekani.

Tukirudi kwa Mgunda ni kwamba walau simulizi za mambo ya jeans zinaweza kutoweka baada ya Simba kutoka sare na Yanga na kisha ikafungwa na Azam. Kwa sasa wanamrudishia ubinadamu wake na watu wanaweza kuhoji masuala ya uwanjani kuliko kuzungumzia mambo ya jeans yake.

Watanzania wengi wataanza kufanya vizuri zaidi pindi kila mmoja atakapoona ana uwezo sawa na raia wa nchi nyingine. Wapo vijana kama Samatta na Diamond ambao wamefikia walipofika sio kwa sababu ya kuwa na vipaji vya ajabu sana, bali kwa sababu waliamini kwamba wapo sawa na raia wa nchi nyingine.

Watanzania wengi hawaamini. Bado tuna vijana ambao ukiwauliza ndoto zao za soka ni zipi watakuambia kucheza Simba na Yanga. Ni wachache wanaoweza kukuambia wanaamini watacheza Manchester United au Real Madrid.

Tukimkumbuka Bob Marley katika wimbo wa Redemption aliwahi kutuambia tujiondoe katika utumwa wa akili kwa sababu hakuna ambaye atakuja kutuondoa katika utumwa huu. Bahati mbaya kila siku linaibuka jambo jipya ambalo linaturudisha katika utumwa wa akili.

Haishangazi kuona leo hatuna watu bora wanaoshindana katika ngazi za kidunia au bara letu. Kila mmoja anajiona hawezi. Kilichobaki ni ushindani wa ndani kwa ndani. Kama akijitokeza ambaye anataka kushindana na wengineo wa nje ya nchi huwa tunaamini kwamba ni Freemason.

SOMA NA HII  BENCHIKHA NI MAFIA SANA AISEE...HIVI NDIVYO ALIVYOINGILIA DILI LA INONGA KUUZWA...