Home Habari za michezo SIKU CHACHE BAADA YA KUFUZU CAF…NABI ALIA NA TFF…ADAI WANAIONEA YANGA KWA...

SIKU CHACHE BAADA YA KUFUZU CAF…NABI ALIA NA TFF…ADAI WANAIONEA YANGA KWA RATIBA NGUMU…

Habari za Yanga

UFINYU wa muda kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa kesho katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza umemuibua Kocha Mkuu wa Yanga, Nasredinne Nabi ambaye amepaza sauti akizitaka mamlaka za soka nchini kutazama upya upangaji wa ratiba ambao hautaziumiza timu.

Nabi amesema timu yake ilikwenda Tunisia kuliwakilisha Taifa na imefanya vizuri lakini mamlaka ni kama hazijazingatia hilo na kuipangia ratiba ambayo ni kama wanaikomoa timu hiyo.

Yanga ilicheza Jumatano nchini Tunisia dhidi ya Club Africain na jana mchana ikarejea nchini na kuunganisha kuja jijini Mwanza ambapo imefika usiku na hadi sasa wachezaji hawajafanya mazoezi kwani Uwanja wa CCM Kirumba una shughuli za kijamii huku Nyamagana ukiwa na mchezo wa Ligi ya Championship kati ya Pamba na Green Warriors.

Kocha huyo raia wa Tunisia ametoa kilio hicho leo katika mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia maandalizi ya kikosi chake kwa mchezo wa kesho, ambapo amesisitiza kuwa muda mwingi wameutumia safarini na kwa siku tatu wachezaji wake hawajarejesha utimamu wa mwili.

“Maandalizi yetu ni magumu hatujapata muda wa kutosha tumetumia muda mwingi kwenye usafiri hilo ni tatizo kubwa kwenye recovery na inaleta mchoko kwa wachezaji. Tunataka tutoe wito kwa viongozi wanaopanga ratiba, wasituadhibu kwasababu tunaliwakilisha Taifa tunaombea siku zijazo lisitokee tena,”

“Lakini tumejiandaa kikamilifu kuelekea mchezo wa kesho tunakwenda kufanya kazi yetu kama tulivyopanga na wachezaji wanaelewa kwahiyo tunatumai tutapata ushindi. Utamaduni wa klabu kubwa kama Yanga ni kujiandaa kila mechi na kuheshimu mpinzani,” amesema Nabi.

Naye Mshambuliaji wa timu hiyo, Yusuph Athuman akizungumza kwa niaba ya wachezaji amesema wanaendelea kuzingatia maelekezo ya timu ya madaktari kuhakikisha wanarejesha utimamu na kuwa tayari kuipatia ushindi timu yao hapo kesho.

Afisa Mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Almasi Kasongo alisema lengo la kutobadilisha ratiba za mechi zao kuepuka viporo.

Kasongo alisema; “Misimu miwili mfululizo tumeshindwa kutekeleza ratiba na mipango kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara tuliyokuwa tunayafanya, Uviko-19 iliingilia kati msimu wa 2020 tukashindwa kumaliza ligi kwa wakati hayo hatutaki yatokee tena msimu huu ratiba itafuatwa hakutakuwa na mabadiliko yoyote.”

SOMA NA HII  CECAFA WAICHOREA RAMANI YA UBINGWA WA LIGI YA MABINGWA AFRIKA SIMBA QUEENS...KILA KITU NI ARUSHA...