Kufuatia vurugu kubwa walizofanyiwa na wenyeji wao mara baada ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Club Africain, uongozi wa Yanga umeweka wazi kuwa tayari umefanya mawasiliano na uongozi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ili kupata taarifa rasmi ya mchezo huo kabla ya kuchukua hatua za kisheria.
Yanga Jumatano iliyopita ilifanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mara baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0, ugenini walipocheza dhidi ya Club Africain nchini Tunisia.
Baada ya mechi hiyo kumalizika Club Africain na kusababisha watu wa usalama kuingilia kati na kuwaondoa Yanga uwanjani chini ya ulinzi mkali.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema: “Ni kweli tumefanya mawasiliano na uongozi wa Shirikisho la Soka Afrika kuomba mapitio ya ripoti ya mechi ili kujua kilichotokea hasa kutokana na mazingira fujo zilizotokea uwanjani.
“Baada ya hapo ofisi ya Ofisa Mtendaji Mkuu itachukua hatua stahiki za kikanuni na kwa kuwa sasa ni mapema sana kulizungumzia hili naomba tuwe watulivu mpaka pale tutakapotoa taarifa rasmi.”