Home Habari za michezo KISA CHAMA… OKRAHA NA PHIRI WAAPA IPO SIKU TIMU MOJA ITAKIONA CHA...

KISA CHAMA… OKRAHA NA PHIRI WAAPA IPO SIKU TIMU MOJA ITAKIONA CHA MOTO..

Chama na Simba SC Msimu Huu

Nyota wa Simba, Augustine Okrah na Moses Phiri wamefichua siri kubwa ya kufanya vizuri msimu huu katika mashindano mbalimbali huku wakibainisha ushindani uliopo kati yao ndio chanzo kikubwa.

Phiri na Okrah wamefunguka kuwa kitu kinachotengenezwa na utatu wao wa Clatous Chama na jeshi zima la Wekundu wa Msimbazi, kuna watu watajua hawajui.

Jeshi la Mgunda juzi lilitoa dozi ya mabao 4-0 dhidi ya Ruvu Shooting huku ‘captain fantastic’ John Bocco akitupia ‘hat-trick’ na kuwa mtu wa pili msimu huu kuondoka na mpira kwenye Ligi Kuu Bara akijibu kile kilichofanywa na straika wa Yanga, Fiston Mayele aliyefanya hivyo Alhamisi dhidi ya Singida Big Stars.

Okrah alisema ushindani uliopo ndani kwa ndani baina yao ndio sababu ya kufanya vizuri kwani kila mmoja wao ana uchu wa mafanikio.

“Ni jambo zuri kuona kila mmoja wetu anapopewa nafasi anaitendea haki, hii inaongeza ari na motisha ya kujituma zaidi kwani bila ya kufanya hivyo unajiwekea mazingira magumu.”

Okrah alisema katika kikosi cha Simba kila mchezaji ni muhimu, hivyo anafurahia ushindani uliopo.

“Ili tutimize malengo ya klabu ni lazima ushindani uwepo na isitoshe hii ni timu kubwa na ndoto ya kila mchezaji kuichezea, naamini kwa mwenendo huu tutafika mbali zaidi ya hapa.”

Simba ndio timu inaongoza kwa kufunga mabao mengi na kuruhusu machache ambapo kwenye Ligi Kuu Bara katika michezo 12 iliyocheza safu yake ya ushambuliaji imefunga 24 na kuruhusu matano.

Kwa upande wa Phiri ameliambia Mwanaspoti kwamba utatu wao utakuja kuwa kitu kikubwa baadaye.

“Sisi wote weledi katika mchezo huu, naamini tutafanya kitu kikubwa kwa ajili ya Simba.”

Kuhusu kukosa mabao katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, Phiri alisema siku ile haikuwa siku yake nzuri.

“Chama ni masta wa kila kitu, anapokuwepo uwanjani na Okrah anatisha pamoja na kukosi kizima,” alisema Phiri.

Straika huyo wa Zambia ndiye mwenye mabao mengi Simba akifunga sita sawa na mastaa wengine kama Idris Mbombo (Azam), Fiston Mayele (Yanga) na Reliants Lusajo wa Namungo.

MGUNDA APIGA SALUTI

Kocha Mgunda amesema kiwango cha wachezaji wake Chama na Bocco kimemfurahisha.

Chama aliyepika mabao mawili hakuwepo kwenye kikosi cha timu hiyo kutokana na kufungiwa mechi tatu na kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi huku Bocco alikuwa sio sehemu ya wachezaji wa kikosi cha kwanza.

Mgunda aliwapa nafasi wachezaji wote hao kuanza baada ya Chama kumaliza kutumikia adhabu yake.

Akizungumzia kiwango cha nyota hao, Mgunda alisema wachezaji hao wamefanya vizuri lakini ni sehemu ya kutimiza majukumu yao.

“Kwa namna moja ama nyingine inawezekana Chama amechagiza ushindi wa leo, lakini sio kwamba alipokuwa hayupo tulikuwa hatushindi,” alisema Mgunda, ambaye timu yake katika mechi zote tatu ilizocheza Simba bila ya kiungo huyo Mzambia timu ilifunga bao moja moja tu.

“Tumecheza mechi tatu akiwa hayupo na tulitoka sare moja na kushinda mbili kwahiyo amekuja na tumeendelea kushinda, Bocco na yeye ametimiza wajibu wake.”

Mgunda alisema; “Chama ni miongoni mwa wachezaji wazuri ambao hawakuwa kwenye kikosi na wamerudi wakitimiza wajibu wao.”

Akizungumzia mabadiliko ya kipindi cha pili akimtoa beki Henock Inonga na kuingia Mohammed Ouattara alisema yalikuwa ya kawaida.

“Inonga hakuumia wala sio kama alicheza vibaya, tulifanya mabadiliko na yalileta majibu mazuri.

Upande wa Kocha wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa akizungumzia mchezo huo alisema walifanya kosa la kuwaruhusu Simba wacheze na waliwaadhibu.

Mkwasa alisema baada ya kufungwa mabao matatu alilazimika abadili mfumo kutoka 3-5-2 na kucheza 4-4-2 lakini bado haikuwa na faida sana.

“Niliwaambia wachezaji wangu tukilegea tutafungwa mabao mengi zaidi, ikabidi turudi kwenye mfumo wetu wa kawaida na tukaingiza beki namba mbili kidogo tukawa tunacheza,” alisema Mkwasa na kuongeza;

“Matokeo haya yanatutoa kwenye kujiamini na ukiangalia tumetoka kutumia nguvu nyingi kwenye mchezo dhidi ya Azam.”

MASALANGA

Kipa wa Ruvu Shooting, Hussein Masalanga ‘Buffon’ amesema wanaobeza uwezo wa Bocco wanatakiwa kuacha kwani ni mchezaji mwenye kipaji anayejua kufunga.

Katika mchezo huo licha ya Masalanga kuonyesha uwezo mkubwa haikuzuia timu yake hiyo kupokea kichapo hicho.

Masalanga ambaye msimu uliopita aliichezea Dodoma Jiji alisema Bocco ni mchezaji wa daraja la juu.

SOMA NA HII  PAMOJA NA UWEPO WA RONADLO....MAN UTD WAINGIA TAMAA DHIDI YA AUBEMEYANGA...WAPANGA KUPINDUA MEZA KIBABE...