Wakati Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ likisubiriwa kutangaza Tarehe mpya na Muda maalum wa Kupanga Makundi Kombe la Shirikisho msimu huu 2022/23, Uongozi wa Young Africans umesema upo tayari kukutanishwa na yeyote kwenye hatua hiyo.
Awali, Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ lilitangaza Makundi ya Michuano ya Kimataifa ngazi ya Klabu yangepangwa Jumatano (Novemba 16), lakini waliakhirisha bila kutoa sababu maalum na kutaja tarehe mpya ya kufanya hivyo.
Young Africans ilifuzu Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika Novemba 09, kwa kuifunga Club Africain bao 1-0 nyumbani kwao Tunis-Tunisia, na kuunga na Klabu nyingine 15 katika hatua hiyo.
Rais wa Young Africans Hersi Said amesema hawahofii kukutana na timu yoyote katika hatua waliyofikia kwenye Michuano ya Kimataifa, hivyo wapo tayari kwa lolote litakalopangwa dhidi yao na ‘CAF’.
Hersi amesema wao kama Young Africans kufuzu hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho lilikuwa ni lengo lao namba moja na kinachofuata kwa sasa ni kuona watafanikiwa vipi, na wala hawahofii timu yoyote kutokana na mipango yao pamoja na ubora wa timu waliyonayo.
“Kwa sasa Young Africans sio Klabu ya kuhofia kukutana na yoyote katika Michuano ya Kimataifa, kwani tuna kikosi bora na pia tuna Uongozi imara ambao naamini ni chachu ya mafanikio makubwa ndani ya klabu yetu, hivyo tupo tayari kwa ajili ya Kombe la Shirikisho na watakaoapangwa na sisi kundi moja.”
“Lengo letu la kwanza lilikuwa ni kufanikiwa kutinga katika Hatua ya Makundi na tunashukuru Mungu kwa kulifikia Lengo letu, ambacho kipo kwa sasa ni kuona nini tutafanikisha kwa kuwa tumejipanga vizuri kufanya makubwa kwenye Michuano ya Kimataifa msimu huu.” amesema Hersi
Young Africans ipo Chungu Namba Mbili, na ina nafasi kubwa ya kupangwa na moja kati ya Klabu za Chungu Namba Moja ambazo ni TP Mazembe (DR Congo), MC Algers (Algeria), Pyramids (Misri) na ASEC Mimosas (Ivory Coast).
Kutoka Chungu Namba Tatu Young Africans itapangwa na moja ya klabu hizi Saint-Elio Lupopo (DR Congo), Al Akhdar (Libya), Real Bamako (Mali) na Rivers United (Nigeria).
Chungu Namba 4 kina Klabu za Diables Noir (Congo Brazzaville), Future (Misri), Marumo Galants (Afrika Kusini) na ASKO Kara (Togo), ambapo moja ya klabu hizo itapangwa kundi moja na Young Africans.