Home Habari za michezo NABI: HUYU MZIZE ATAIMBWA SANA HAPA YANGA…AFUNGUKA KILICHOMPATA MAYELE…

NABI: HUYU MZIZE ATAIMBWA SANA HAPA YANGA…AFUNGUKA KILICHOMPATA MAYELE…

Habari za Yanga

KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi amekiri kufanya mazungumzo na Clement Mzize kabla ya mchezo wa mchezo wa Kagera na kumsisitiza chipukizi huyo kuwa yeye ni mashine, ajiamini na akakiwashe dhidi ya Kagera Sugar.

“Kabla ya mchezo nilikaa naye na kumpa maelekezo nashukuru amefanya kitu kizuri, alichokifanya ameonyesha ubora maradufu akinipa wakati mgumu wa kunifikirisha ni namna gani nitaweza kumtumia kwenye michezo iliyobaki,” alisema na kuongeza;

“Mzize ni mchezaji mzuri mpambanaji na sahihi kwenye eneo analocheza kutokana na umbo lake na mikimbio yake uwanjani namuona mbali atakuja kuwa staa wa Tanzania eneo la ushambuliaji kama ataendeleza ubora wake alioanza nao,”alisema akimzunguzia staa huyo aliyetupia bao pekee la ushindi dhidi ya Kagera.

Nabi alisema ataendelea kumtumia kadri muda unavyozidi kwenda kulingana na mahitaji ya uwepo wake kwenye michezo iliyobaki ya ligi na ikimpendeza zaidi ataweza kumtumia hadi kwenye mashindano ya kimataifa ambayo Yanga ni wawakilishi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya Makundi.

KUHUSU FISTON MAYELE

Wakati kinara wa mabao msimu uliopita wa Yanga, Fiston Mayele akishindwa kuonyesha makeke yake ya kufunga katika mechi saba alizocheza kocha wake Nasreddin Nabi amesema staa wake huyo amechoka lakini atakaa sawa na kufunga.

Mayele ametumia dakika 366 ndani ya kikosi hicho msimu huu bila kutetema baada ya kushindwa kufunga bao hata moja kwenye mechi tano za ligi Kuu Bara na mbili za kimataifa.

Mayele ambaye amecheza dakika 562 kwenye mechi nane alizocheza mara ya mwisho aliifunga Mtibwa Sugar kwenye ushindi wa mabao 3-0 mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Mshambuliaji huyo amecheza mechi nane kati ya tisa zilizochezwa na timu yake na kukusanbya pointi 23 zinazowafanya waongoze Ligi Kuu Bara msimu huu wao wakiwa ndio mabingwa watetezi.

Alianza kucheza dhidi ya Polisi Tanzania dakika (86), Coastal Union (20), Azam FC (90), Mtibwa Sugar (90), Ruvu Shooting (83), Simba (90), Geita Gold (13) na mchezo dhidi ya Kagera Sugar alicheza dakika 90.

Kwenye mechi hizo amefunga dhidi ya Polisi Tanzania, Coastal Union na Mtibwa Sugar zote akizifunga bao moja moja huku michezo mingine mitano akikosa nafasi ya kufunga.

Nabi alimkingia kifua mshambuliaji huyo akisisitiza kuwa ataendelea kumtumia kwasababu anamuamini na ndiye mshambuliaji ambaye ameshathibitisha ubora wake ndani ya timu na ligi hiyo.

“Mayele ni mchezaji mzuri na mkubwa anapitia wakati mgumu tu kwa sasa ambayo ni wachezaji wengi wakubwa wanaupitia bado ananafasi ya kufanya vizuri nitaendelea kumtumia kwenye mechi zilizo mbele yetu,” alisema na kuongeza;

“Alikuwa ni mfungaji bora msimu uliopita uwepo wake tu uwanjani unaongeza nguvu na pamoja na kutokufunga amekuwa bora kwenye majukumu ambayo nimekuwa nikimpa ayafanye ni suala la muda atafunga na atarudi kwenye ubora ambao amekuwa akiuonyesha tangu ametua Tanzania.”

Alisema anajukumu kubwa la kuzungumza naye kwenye uwanja wa mazoezi ili kurudisha kwenye utulivu kiwanjani na kuweza kutumia kila nafasi anazotengenezewa anaamini hilo linawezekana mchezaji huyo kuendelea pale alipoishia.

Nabi alisema amebaini ukame wa mabao kwa staa huyo na ndio maana amekuwa akibadilisha mfumo kwa kuwachezesha washambuliaji wawili akiamini kuwa asipofunga yeye mchezaji mwingine atafunga.

“Kama kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar niliwatumia washambuliaji wawili na matunda yameonekana Mayele kashindwa kufunga Clement Mzize amefunga na kuipa timu bao la ushindi.”

MSIKIE MZIZE

“Kwanza nilipoambiwa naanza kiukweli nilishtuka sana nikajiuliza naanzaje Leo wakati wa mechi ngumu kama hii alafu hali ya hewa ya mvua lakini makocha wangu kocha Nabi akaniambia sana kwamba nisiwe na presha kabisa wala nisiogope nikacheze tu kuonyesha uwezo wangu,”alisema Mzize.

“Hata kocha Kaze naye akaniambia hivyo hivyo nijiamini nilishukuru zaidi wachezaji wenzangu kaka zangu walinifuata na kuniambia nijiamini nikatulie na kufunga kama ambavyo nafanya mazoezini.

“Ile krosi ilipokuja kwa kuwa tulishapewa maelekezo niliona jinsi Feisal anavyokimbia nikasema acha niifuatilie na kwa jinsi mabeki wa Kagera walivyokaa ilikuwa lazima ije vile nikajiweka sehemu sahihi nikapiga kichwa kile,nilijua kwamba kama atapiga vile basi nitafunga.

Aidha Mzize alisema alipopangwa kucheza sambamba na Fiston Mayele haraka Mkongomani huyo alianza kumsuka kwa wao kucheza kwa mkakati wa jinsi ganj ya kupishana na kucheza maeneo ya kufunga.

“Unajua wakati tuko kwenye kikao cha mechi tulishaelekezwa jinsi tubavyotakiwa kucheza kwa hesabu kati yangu na Mayele na hata tulipokuwa uwanjani Mayele alikuwa ananisaidia sana.

“Alikuwa anajua Kuna wakati mabeki watamfuata sana yeye basi Mimi nikimbie maeneo ya kufunga na hiki ndicho tulichokitumia kupata lile bao.

“Kiukweli najifunza mengi sana kwa Mayele, huyu ni mshambuliaji bora kwenye timu yetu, lakini pia wako kaka zangu wengine kama kina Yusuf Athuman na wengine nao wamekuwa wakiniboresha sana nje ya makocha.

“Muda ambao makocha wamekuwa wananipatia utaendelea kunijenga zaidi na najua kwamba bado Nina safari ndefu ya kuendelea kupambana na sitaki kukata tamaa wala kuridhika.”

SOMA NA HII  WAKATI WAKIHAHA NA KOCHA....ANTONIO CONTE ATUMA UJUMBE HUU KWA AZAM FC YA BONGO...