Straika wa kimataifa wa zamani wa Tanzania aliyewahi kuwika Nazareth Njombe na Simba, Emmanuel Gabriel ‘Batgol’ amesema lazima nahodha wa Simba, John Bocco apewe heshima kutokana na mchango kwa klabu hiyo, licha ya sasa kutopata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.
Mkongwe huyo alisema Bocco, hatendewi haki na timu hiyo na sasa inapaswa aheshimiwe kwa mchango mkubwa alioufanya kwa kipindi chote alichotua Msimbazi akitokea Azam FC.
Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na gazeti la Mwanaspoti, Batgol alisema Bocco ni miongoni mwa mastraika wenye uwezo mkubwa zaidi kutokana na nafasi anayocheza kwani anapopata nafasi ya kucheza anafunga na msimu huu ana mabao manne.
Bocco ndiye mchezaji anayeshikilia rekodi kwa sasa ya kucheza misimu 15 ya Ligi Kuu Bara mfululizo na kufunga kila msimu akiwa na mabao 146 kwa sasa, yakiwamo 88 aliyofunga akiwa Azam aliyoipandisha daraja mwaka 2018.
“Inawezekana watu wanamchukulia poa, lakini mchango wa Bocco kwa Simba na soka la Tanzania kwa jumla ni kubwa na anapaswa kuheshimiwa kwanza klabuni, tangu alipotua akishirikiana na wenzake ameibeba mno timu, ikiwamo kubeba mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu,” alisema.
Mbali na hilo, Batgol aliutaka uongozi wa Simba kutuliza upepo mbaya unaoendelea ndani ya klabu ambao unaweza kusababisha anguko kwa timu yao huku akishauri kuhakikisha wanasajili sehemu muhimu katika dirisha dogo la usajili unaotarajia kufunguliwa Desemba 15 mwaka huu.
Alisema sehemu ya kwanza ni kutafuta straika namba tisa asilia kama alivyo Bocco ambaye kipindi hiki ameonekana kutofanya vizuri mechi mfululizo.
“Moses Phiri ndiye ana uwezo mkubwa wa kufunga lakini sio namba tisa asilia kama ilivyo kwa Bocco ingawa hawamtendei haki, Bocco anafunga kama nilivyokuwa nafunga mimi, anapoingia kipata nafasi anafanya kweli ila wao ndio wanamtoa kwenye mchezo, sasa asajiliwe mwenye ubora zaidi wa Bocco.
“Pia atafutwe namba nane asilia ambaye ni mtaalamu wa kupiga pasi za mwisho sio kama ilivyo kwa Chama ambaye ni namba 10, asipokuwepo inakuwa shida ndani ya timu, hata namba mbili na tatu wa kuwapa changamoto Shomary Kapombe na Mohammed Hussen ‘Tshabalala’,” alisema na kuongeza
“Kuna Israel Mwenda na Gadiel lakini naona wameshindwa kuwapa changamoto Kapombe na Tshabalala ingawa ni wachezaji wazuri, sijui kitu gani kinawapata, vile vile namba 6 maana Jonas Mkude yupo kama Bocco siku hizi, Kennedy Juma apewe nafasi ya kucheza ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa ila hathaminiwi ndani ya timu.”
Kuhusu nafasi ya timu yake msimu huu, Batgol alisema; “Nasisitiza tena kama viongozi wasipotulia basi nafasi ya kwanza na ya pili kwenye Ligi Kuu wataitafuta sana, kwenye uongozi kuna vitu havipo sawa, wakae na wachezaji watatue hili jambo la wazawa kudharauriwa huku wakithaminiwa wageni.”
Stars huyo alizungumzia maisha yake mapya ndani ya Fountain Gate FC akiwa meneja wa timu hiyo alisema; “Naamini hii timu itapanda Ligi Kuu msimu ujao, maana ina kila kinachotakiwa kwa mchezaji na benchi la ufundi kinapatikana.” Mwanaspoti. Kata kiu ya michezo na