Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Nasreddine Mohamed Nabi amesema ana matumaini makubwa kikosi chake kitafanya vizuri Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika, baada ya kuwafahamu wapinzani.
Young Africans juzi Jumatatu (Desemba 12) ilipangwa Kundi D na klabu za TP Mazembe (DR Congo), Real Bamako (Mali) na US Monastir (Tunisia).
Kocha huyo amesema anaziheshimu timu zote walizopangwa nazo kwenye Kundi hilo, lakini anaamini kikosi chake kina nafasi kubwa ya kuvuka hatua hiyo, kama ilivyo kwa timu nyingine.
Amesema hadi sasa kila timu ina uwezo wa kwenda Hatua ya Robo Fainali kwa sababu hadi kufika Hatua ya Makundi kuna ubora na upambanaji iliyoonesha katika hatua zilizopita, na ndio maana zipo hapo.
“Nafasi iko wazi kwa timu zote, tunakwenda kushindana na timu zenye uzoefu na uwekezaji mzuri lakini nafasi bado iko wazi.
“Tuna kikosi kizuri na tutakuwa na maandalizi mazuri ya kujiandaa kwenye hatua hii, naamini tutafanya vizuri na tutafuzu,” amesema Kocha Nabi.
Young Africans itaanzia ugenini Tunisia kwa kucheza dhidi ya US Monastir na mchezo wa pili itacheza nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.
Mchezo wa tatu wababe hao wa Jangwani watasafiri kuelekea Mali kupambana na Real Bamako, kabla ya timu hizo kucheza tena katika mchezo wanne jijini Dar es salaam.
Young Africans itaendelea kusalia nyumbani katika mchezo wa tano, ikicheza dhidi ya US Monastir ya Tunisia, kisha itakwenda kumalizia michezo ya Hatua ya Makundi mjini Lubumbashi-DR Congo kwa kuikabili TP Mazembe.