Home Habari za michezo HAWA HAPA WACHEZAJI KUMI NA MOJA AMBAO WAPO WAPO TU …WACHEZE, WASICHEZE...

HAWA HAPA WACHEZAJI KUMI NA MOJA AMBAO WAPO WAPO TU …WACHEZE, WASICHEZE HAKUNA ANAYEJALI…

Ligi Kuu Tanzania 2023/24

Utamu wa Ligi Kuu Bara unarejea tena leo kwa mechi za ufunguzi wa mzunguko wa pili, Ruvu Shooting ikicheza dhidi ya Ihefu na KMC ikiikaribisha Coastal Union ya Tanga.

Mambo yalikuwa ni mengi katika mzunguko wa kwanza. Kuna wachezaji walikiwasha ile mbaya na kujenga heshima kubwa kwa mashabiki wao na kuna wengine hao ambao mambo yao hayakuwa poa kabisa, hawakupata muda wa kutosha wa kucheza na kujikuta wakipachikwa majina ya utani mitandaoni yakiwamo ya watumishi hewa.

Makala hii inakuletea kikosi cha wachezaji ambao wamekula mishahara yao ya nusu msimu huku wakitumia sehemu kubwa ya msimu wakiwa benchini ama jukwaani kwenye vikosi vya Simba, Yanga na Azam.

Erick Johora

Kipa chaguo la tatu Yanga, Johora alianza kikosini Jumapili iliyopita wakati timu yake ikishinda 8-0 dhidi ya Kurugenzi ya Simiyu katika mechi ya hatua ya 64-Bora ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Lakini hiyo ilikuwa ni mechi yake ya kwanza kutumika langoni kwa kipindi cha takriban mwaka mzima tangu mara ya mwisho alipocheza mechi ya kimashindano msimu uliopita kwenye Kombe la Mapinduzi lililofanyika visiwani Zanzibar kati ya Desemba 2021 na Januari 2022.

Johora, ambaye alitarajiwa kufanya makubwa wakati aliposajiliwa kutokea katika klabu ya Aigle Noir ya Burundi, amekuwa akiishia jukwaani na wakati mwingine anapokosekana Djigui Diarra, langoni huanza Aboutwalib Mshery na kwenye benchi ndio atakaa Johora.

Kwa upande wa Simba, kutokana na ubora wa makipa Aishi Manula ambaye ndiye chaguo la kwanza na Benno Kakolanya aliye chaguo la pili, kumemfanya kipa chaguo la tatu, Ally Salim kuishia benchini ama jukwaani na kushindwa kucheza mchezo wowote wa ligi hadi mzunguko wa kwanza ulipomalizika.

Erasto Nyoni

Beki wa kulia kwenye kikosi hiki atakuwepo kiraka wa Simba, Nyoni. Huyu mwamba alikuwamo katika kikosi cha Taifa Stars kilichoipasua timu ya taifa ya Morocco 3-1 katika mechi ya kuwania kufuzu ushiriki wa Kombe la Dunia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa mwaka 2013.

Nyoni ndani ya Simba licha ya kuwa na sifa ya kucheza kwenye nafasi nyingi kiwanjani, amekuwa mchezaji chaguo la tatu katika kila nafasi ambako kuna wachezaji wawili ambao hutumika zaidi.

David Raphael

Tangu msimu huu umeanza nafasi ya beki wa kushoto Yanga wamekuwa wakicheza wachezaji wawili tofauti huku, Raphael akiwa chaguo la tatu mbele ya Joyce Lomalisa na Kibwana Shomary.

Lomalisa kwa sasa amekuwa kwenye kiwango bora katika nafasi hiyo ila muda mwingine hutumika Kibwana na kama ikitokea wote wamekosekana, Farid Mussa hucheza hapo huku Raphael kuishia benchi au kuwa jukwaani kabisa.

Abdallah Shaibu ‘NINJA’

Aliongezewa mkataba na Yanga kwenye dirisha kubwa la usajili msimu huu, lakini alishindwa kuwa mchezaji tegemeo mwanzoni, akatolewa kwa mkopo Dodoma Jiji.

Tangu alipocheza mechi ya Dodoma Jiji dhidi ya Simba na kujifunga bao katika kipigo cha 3-0, Shaibu amekuwa haonekani uwanjani na hapati nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho tofauti na ilivyokuwa ikifikiriwa na wengi.

Nassoro Kapama

Simba ilimsajili kama mchezaji kiraka kwenye dirisha kubwa la msimu huu na kuna nyakati mwanzoni alikuwa akipata nafasi ya kucheza kwenye baadhi ya mechi ila sasa haonekani uwanjani.

Kapama katika kila eneo analoweza kucheza amekuwa mchezaji chaguo la nne. Katika kikosi hiki atacheza nafasi ya beki wa kati pamoja na Shaibu.

Cleophas Mkandala

Alikuwa kiungo wa kocha, Abdihamid Moallin kikosini Azam kwenye mechi za mwanzoni wa msimu na hata chini ya kocha aliyefuatia, Denis Lavagne ilicheza ingawa kwa dakika chache.

Hivi sasa Azam ikiwa chini ya kocha, Kally Ongala, Mkandala amekuwa mchezaji wa kuishia benchini au jukwaani kwani eneo la kiungo wanaotumika zaidi ni Issah Ndala na James Akaminko.

Shabani Chilunda

Winga wa kulia kwenye kikosi hiki atacheza Chilunda, staa wa Azam.

Chilunda alikuwa na majeraha ya goti yaliyomsumbua kwa muda mrefu ila hata baada ya kupona amekuwa hapati nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Azam licha ya kwamba yamefanyika mabadiliko ya makocha watatu.

Nelson Okwa

Kutokana na ubora wake alionyesha na kikosi cha Rivers United ya Nigeria msimu uliopita aliwavutia mabosi wa Simba kumsajili ila mambo yamekuwa tofauti kwake ndani ya timu yake mpya akishindwa kung’aa.

Okwa alianza vizuri maisha ndani ya Simba ikiwemo kufunga bao kwenye mechi ya kirafiki siku ya kilele cha Simba Day dhidi ya St. George ya Ethiopia, lakini amepotea.

Mwingine ni Ibrahim Ajibu ambaye amekuwa mchezaji wa kuishia benchini au jukwaani, akicheza kwa dakika chache Azam FC.

Heritier Makambo

Msimu uliopita alisajiliwa kwa matumaini makubwa ndani ya kikosi cha Yanga kutokana na makubwa aliyowahi kufanya kwenye timu hiyo kabla ya kutimkia, Horoya ya Guinea ambako alishindwa kung’aa.

Aliibeba Yanga ikienda kutwaa Kombe la ASFC msimu uliopita, lakini kwenye ligi mambo yamegoma.

Yusuph Athumani

Mshambuliaji wa Yanga tangu msimu uliopita alisajiliwa akitokea Biashara United amekuwa hapati nafasi ya kucheza kama ilivyokuwa msimu huu ameingia kwenye michezo miwili hata dakika kumi hazifiki.

Alifunga mabao mawili akiingia kutokea benchini katika mechi ya ASFC waliyoshinda 8-0 dhidi ya Kurugenzi Jumapili, lakini kwenye ligi anaonekana kupitwa na hadi kinda Clement Mzize.

Crispin Ngushi

Hadi mzunguko wa kwanza unamalizika hajacheza mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

MAKOCHA WANENA

Kocha wa Dodoma Jiji, Mellis Medo anasema timu kubwa kuna wachezaji wengi wazuri ila ushindani unakuwa mkubwa hadi wengine kushindwa kupata nafasi ya kucheza na kuonekana kama wapo wapo tu.

“Hadi Simba, Yanga na Azam zinakuwa na huyo mchezaji kwenye kikosi basi yupo na kitu cha ziada haswa katika ubora wake ila inakuwa bahati mbaya anashindwa kufanya vizuri na kupata nafasi ya kucheza,” anasema Medo.

Kocha wa Polisi Tanzania, Mwinyi Zahera anasema thamani ya mchezaji katika timu aliyopo ni kupata nafasi ya kucheza na kutoa mchango wake kulingana na ubora uliofanya awepo kwenye timu.

SOMA NA HII  KISA SIMBA SC KUTOLEWA CAF....YONDANI AIBUKA NA HILI JIPYA...AITAJA YANGA SC...