Home Habari za michezo MOGELLA:- CHAMA ANAENDELEZA UFALME WAKE SIMBA SC…HATA OKWI ALIFANYA…

MOGELLA:- CHAMA ANAENDELEZA UFALME WAKE SIMBA SC…HATA OKWI ALIFANYA…

Chama na Simba SC Msimu Huu

Kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Clatous Chama ameweka rekodi yake Ligi Kuu akihusika kwenye mabao mengi, huku nyota wa zamani wa timu hiyo, Zamoyoni Mogella akisema anachokifanya nyota huyo ni kuendeleza ufalme wake.

Chama ambaye kwa sasa ndiye kinara wa pasi za mabao Ligi Kuu akiwa nazo tisa na mabao matatu baada ya michezo 16, pia ana uwezo wa kucheza kama kiungo wa pembeni na amevunja rekodi ya Abrahman Mussa na Reliants Lusajo ambao walimaliza na pasi sita kila mmoja msimu uliopita.

Chama amekuwa mhimili mkubwa kwenye mabao ya Simba SC akitumia uhodari wake wa kuwatoka mabeki wa timu pinzani na chenga za maudhi huku miguu yake ikiwa ya dhahabu kupiga pasi za mwisho.

Mshambuliaji huyu raia wa Zambia kabla hajaondoka nchini kwenda kucheza soka la kulipwa RS Berkane ya Morocco, msimu wa 2020/21, alimaliza na pasi za mabao 10 na kufunga mabao saba.

Kwa maana hiyo, tangu aondoke nchini hakuna mchezaji aliyefikia rekodi yake ya kupiga pasi za mwisho Ligi Kuu, lakini kumbukumbu ya pasi nyingi nyuma yake zilipigwa na Ibrahim Ajib akiwa na Yanga msimu wa 2018/19, asisti 14.

Hata hivyo, Chama msimu huu inaonekana anaweza akafanya vizuri zaidi kwani ndio kwanza mzunguko wa pili wa ligi kuu uimeanza.

MSIKIE MOGELA Nyota wa zamani Simba SC na Yanga SC, Mogela alizungumzia kiwango cha Mzambia huyo, kinatokana na ubora alionao, pia inawezekana kuna wepesi kwenye ligi yetu.

“Amejiweka sehemu ile ile, ni jambo zuri kwa sababu ameondoka na ufalme wake na amerudi kuuendeleza. Ni kama ilivyokuwa kwa Okwi (Emmanuel). Chama kule Morocco hakufanya hivi, ni kama ilivyokuwa kwa Okwi baada ya kuondoka. Hii inaonyesha inawezekana hapa kuna wepesi,” alisema.

Mshambuliaji wa zamani Simba SC, Bakari Kigodeko alisema Chama ni mchezaji wa kuigwa kwa sababu kiwango chake kimeendelea kuwa juu.

“Anafanya vizuri ndani ya ligi na hata nje, Simba SC inafaidika naye kwa sababu anafunga na kutoa pasi za mabao kwa wenzanke.”

SOMA NA HII  HAYA HAPA MAAJABU YA MGUNDA SIMBA...WAKONGWE WAMPIGIA SALUTI