KIUNGO kutoka Burundi aliyewahi kukipiga Newcastle United ya England, Gael Bigirimana ni kama ameishika pabaya Yanga SC iliyokuwa ikipiga hesabu za kumtema, lakini ikibanwa na mkataba uliopo ambao utawalazimisha waajiri wake kumlipa mkwanja mnono.
Awali ilielezwa Yanga SC ilikuwa na mpango wa kumpiga chini Bigirimana kupitia dirisha dogo la usajili kutokana na kushindwa kuonyesha makeke yaliyotarajiwa, lakini inadaiwa hesabu hizo zimekufa.
Awali, Yanga SC ilikuwa ikiwaza kumtoa Bigirimana kwa mkopo au kuvunja mkataba wake kutokana na kutoridhishwa na kiwango chake ili kusajili wachezaji wengine wapya wa kigeni kutokana na idadi ya ‘mapro’ (12), kutimia kikosini hapo.
Wachezaji wengine waliokuwa katika hesabu hizo ni Heritier Makambo, Tuisila Kisinda na Jesus Moloko, lakini ghafla Bigirimana ameondolewa kwenye mipango hiyo baada ya vigogo kuangalia mkataba wake na kuona unahitaji pesa nyingi ili kuuvunja.
Taarifa zinasema kuwa katika mkataba wa miaka miwili aliousaini Bigirimana mwanzoni mwa msimu huu ili kuuvunja, Yanga SC inahitaji kumlipa nyota huyo zaidi ya Dola 300,000 ambazo ni zaidi ya Sh750 Milioni.
Pesa hiyo imeonekana kuwaumiza vichwa viongozi wa Yanga SC na kuamua kumuacha kiungo huyo abaki na sasa panga limebaki kuwalenga Makambo, Kisinda na Moloko.
Watatu hao mmoja atampisha Yacouba Songne ambaye ataanza kukiwasha kwenye Kombe la Mapinduzi linaloanza kesho visiwani Zanzibar na wengine watawapisha mastaa wapya wawili walio mbioni kusajiliwa.
Lakini pia huenda mabosi wa Yanga SC wakabadili mawazo na kuachana na usajili wa dirisha dogo hili na kuvuta kasi kwaajili ya msimu ujao.
Hakuna kiongozi yeyote wa Yanga aliyepatikana kwa vile simu zao zilikuwa zikiita bila kupokewa.