WAKATI mshambuliaji wa zamani wa TP Mazembe ya DRC na Timu ya Taifa (Taifa Stars), Thomas Ulimwengu, akitajwa anakaribia kutua Jangwani, mabosi wa Yanga wamesema usajili wao utakaofuata ‘utatingisha’ kwa sababu wanahitaji kutetea ubingwa wa Bara na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Tayari Yanga imeshamtambulisha kiungo, Mudathiri Yahya kutoka KMKM ya visiwani hapa huku ikiweka wazi inahitaji kupata mshambuliaji mpya.
Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, alisema kuwa kabla ya dirisha dogo la usajili halijafungwa, klabu hiyo itatangaza usajili mkubwa na kuongeza kwa sasa wako katika hatua za mwisho za mazungumzo na nyota hao.
Haji alisema baada ya kufanikiwa kuwaongeza mikataba baadhi ya wachezaji wao akiwamo kipa, Djigui Diarra, Khalid Aucho na Dickson Job sasa nguvu wanazielekeza kwa nyota wapya ambao ujio wao utasaidia kuimarisha kikosi chao.
“Kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili tutashusha majina mawili mapya mazito, usajili tunaoufanya ni mapendekezo ya benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha wetu, Nesreddine Nabi, kwa kutuelekeza tufanye usajili wa aina gani kulingana na maeneo aliyoyaelekeza. Muda wowote ndani ya hizi siku 10 tutatangaza majina ya wachezaji hao na kufunga usajili wetu,” alisema bosi huyo.
Aliongeza kila usajili unaofanywa unalenga kuziba makosa na madhaifu yaliyoko na wanaamini utaimarisha zaidi ubora wa kikosi chao hasa katika safu ya ushambuliaji ambayo kwa sasa inaongozwa na kinara wa mabao, Fiston Mayele.
“Kurejea kwa wachezaji wetu wawili, Yacouba Songne na Lazarous Kambole, ambao tunawaona katika mashindano haya ya Mapinduzi wakicheza, hii ni faraja, itawasaidia kurejea katika ubora wao,” aliongeza Haji.