Home Habari za michezo KUHUSU MASTAA WANAOKATWA YANGA…UKWELI WA MAMBO UKO HIVI…ATAKAYEPONA NI HUYU…

KUHUSU MASTAA WANAOKATWA YANGA…UKWELI WA MAMBO UKO HIVI…ATAKAYEPONA NI HUYU…

Habari za Yanga

Wakati Yanga ikitajwa kuwa inaweza kushusha majembe mengine matatu mapya kwenye dirisha hili la usajili, vita imehamia kwa wachezaji wanaoweza kukatwa.

Yanga inakaribia kumalizana na mshambuliaji Mzambia, Kennedy Musonda aliyebakiza hatua chache kutambulishwa lakini mpango huo unawapasua vichwa viongozi wa timu hiyo kutokana na idadi ya mastaa kutoka nje ya nchi kuzidi 12, ambayo inatakiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na jana walijifungia kujadili.

Wachezaji wa kigeni wa Yanga ni, Djigui Diarra, Djuma Shaban, Joyce Lomalisa, Yanick Bangala, Gael Bigirimana, Khalid Aucho, Stephen Aziz Ki, Tuisila Kisinda, Jesus Moloko, Benard Morrison, Fiston Mayele na Heritier Makambo huku kambini kukiwa na wengine wawili, Lazarous Kambole na Yacouba Songne ambao wapo kwenye uangalizi maalumu.

Inafahamika kuwa Yanga ipo kwenye hatua za mwisho kuachana na Makambo na nafasi yake awali ilielezwa ingezibwa na Yacouba aliyetoka kwenye majeraha ya muda mrefu lakini kiwango chake kwenye Kombe la Mapinduzi kimewapa wasiwasi viongozi Yanga na kuanza kupanga kumtoa kwa mkopo.

Wakati huohuo, Kambole naye hajawashawishi viongozi wa Yanga na benchi lake la ufundi na sasa wanawaza kuachana naye, lakini hata hivyo wakiondoka Kambole na Yacouba ambao hawapo kwenye usajili, ambaye ana asilimia kubwa za kutoka ni Makambo na nafasi yake itazibwa na Musonda.

Jambo hilo limewafanya viongozi wa Yanga na benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Nassredine Nabi jana kuwa na vikao visivyoisha kwani ‘Profesa’ huyo anataka majembe matatu ambayo mmoja ni Musonda na mwengine ni beki kisiki wa kati na kiungo mmoja mwenye uwezo wa kucheza maeneo tofauti uwanjani.

Vikao hivyo, ambavyo vilianza jana vinajadili kwa kina ni nani wamtoe kikosini na ubora wa wachezaji wapya wanaopanga kuwasajili na moja kwa moja majina ya Gael Bigirimana, Makambo, Jesus Moloko, Tuisila Kisinda na Djuma Shaaban ndiyo yako mezani kupunguza wawili hadi watatu kati ya hao.

Yanga ipo tayari kuachana au kumtoa kwa mkopo Bigirimana kutokana na kushindwa kuonyesha kiwango bora kikosini hapo, lakini ugumu unakuja mchezaji mwenyewe hayupo tayari kutoka kwa mkopo na kama kuondoka, basi wavunje mkataba ambao Yanga italazimika kulipa 300,000 dola ambazo ni zaidi ya 700 milioni za Kitanzania, hivyo kufanya jambo lake kuondoka kuwa gumu na huenda akasalia mitaa ya Jangwani.

Kisinda yupo Yanga kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea RS Berkane ya Morocco na huenda akabaki Jangwani hapo kwani Yanga haitumii gharama kubwa kumtunza kutokana na kuwa na mkataba na Berkane ikiwemo kiasi kadhaa cha mshahara wake.

Djuma ameingia kwenye orodha hiyo kutokana na kushuka kwa kiwango chake na hivi karibuni amekuwa akiishia benchi na wakati mwingine kukaa jukwaani na nafasi yake kuchukuliwa na Kibwana Shomari lakini bado kunakuwa na ugumu wa kumuachia kwani alifanya vizuri mwanzoni na Kocha Nabi anaamini atarejea kwenye ubora wake na kuisaidia timu.

Ubora wa Moloko aliounyesha ndani ya Yanga nao unaongeza ugumu wa kufanya maamuzi kwa viongozi wa Yanga kumtoa na hivyo kubaki wakiwaza wanamtoa nani na abaki nani.

Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said, alisema Yanga itasajili wachezaji wachache na bora ili kuhakikisha inakuwa imara na kutetea ubingwa wa ligi iliouchukua mara 28, sambamba na kufanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

“Tutafanya maboresho madogo kwenye kikosi chetu katika dirisha dogo kwa kufuata matakwa ya benchi la ufundi ili kuwa imara na kufikia malengo, tuweze kushindana na timu kubwa na kufanya vizuri ni lazima uwe na kikosi kipana na chenye wachezaji wenye utayari wa kupambana,” alisema Hersi aliyechaguliwa mwaka jana kuwaongoza Wananchi.

“Nahitaji wachezaji wasiozidi watatu kwenye dirisha hili dogo, mshambuliaji wa kusaidiana na Mayele ni muhimu sana lakini pia naangalia uwezekano wa kuongeza beki na kiungo ambao watakuwa na uwezo zaidi wa kucheza nafasi tofauti uwanjani,” alisema Nabi.

Hadi sasa Yanga imekamilisha usajili wa kiungo mzawa, Mudathiri Yahya (huru), na kabla ya hapo amewahi kuzichezea KMKM ya Zanzibar, Singida United na Azam kwa mafanikio makubwa lakini pia imemtoa mshambuliaji wake Yusuph Athuman kwa mkopo wa miezi sita kwenda Coastal Union.

SOMA NA HII  KISHA USHINDI WA YANGA SC CAF....MZEE YUSUF ASHINDWA KUJIZUIA....AFUNGUKA HAYA KWA WANIGERIA....