Nyota wa Simba, Kibu Dennis ameeleza siri ya kumkosha kocha wake, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambaye alishindwa kujizuia Dubai walipoweka kambi na kutoa zawadi kutokana na makubwa anayoyafanya kwenye mazoezi.
Robertinho alianza kuvutiwa na Kibu tangu wakati wa Kombe la Mapinduzi ambapo Simba iliishia kwenye hatua ya makundi kutokana na staili ya uchezaji wake ambapo amekuwa akisifika kuwa na spidi na nguvu wakati akishambulia lakini pia ni mwepesi wa kusaidia kuzuia mashambulizi.
“Kila mchezaji anatamani kuwa na kiwango bora, iko hivyo kwangu pia na ili kufanikisha hilo najitahidi kujituma na kufanya mazoezi kwa bidii kuhakikisha natoa kila nilichonacho kwa timu,” alisema Kibu na kuongeza;
“Sio kwamba mimi ni bora kuliko wote lakini najitahidi kufuata maelekezo na kufanya vile ambavyo makocha wanataka nifanye nadhani ndio sababu kocha kaamua kunipa zawadi.”
Akiongelea zawadi hiyo, Robertinho ambaye huo ni utaratibu wake kutoa zawadi kwa mchezaji anayemkosha alisema, “Wakati huu wa maandalizi, tumekuwa na maandalizi ya nguvu kila siku, tumekuwa tukifanya sana kazi, kama mchezaji anafanya vizuri ni jambo jema kumpongeza kwa zwadi.”
Kwa upande wa Fred Felix ‘Minziro’ kocha wa kwanza kumnoa Kibu kwenye soka la ushindani akiwa Geita Gold kipindi ipo Daraja la kwanza alisema Kibu ni mpambanani na hilo litamsaidia kufika mbali.
“Kibu anapambana sana, ni miongoni mwa wachezaji wenye njaa ya mafanikio. Hana mambo mengi ni msikivu hivyo kila anachoelekezwa mara nyingi anakifanyia kazi na kuongeza juhudi zake binafsi kuhakikisha kila kitu kina kwenda sawa,”
“Kama ataendelea hivyo atafika mbali kwani makocha wengi wanapenda wachezaji wasikivu na wapambanaji,” alisema kocha huyo.