Baada ya kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF kuthibitisha kuwa kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ ana mkataba halali na Yanga maoni na mitazamo ya watu ilikuwa mingi sana
Kuna watu wanaamini kuwa kwenye sakata hili Feisal ameonewa lakini kuna wengine wanaamini kuwa Feisal anastahili kuendelea kuutumikia mkataba wake mpaka utakapomalizika
Soka letu limejaa siasa za ajabu sana na inaaminika kuwa Feisal anasukumwa na baadhi ya watu kufanya anachokifanya bila kujali kiwango chake au athari anayoipa klabu kwa sasa.
Bado ni kijana mdogo sana anahitaji kuendelea kupambania kipaji chake ili kuendeleza maisha yake ya sasa na ya baadae, ni wazi kuwa vipengele vya mkataba vimembana na mpaka sasa ni mchezaji wa Yanga na alipaswa kuwa anatumikia klabu yake
Baadhi ya mashabiki wa Yanga wamechukizwa sana na namna kiungo huyo Mzanzibar alivyowaaga akionyesha nia ya kuondoka kabisa Jangwani
Feisal bado ni mchezaji wa Yanga kwa mujibu wa TFF na uwezekano wa kumaliza tofauti hizi bado upo ili arejee kuipambania klabu na kipaji chake pia
Kwa sasa wengi wanaweza kuona Feisal hahitajiki tena lakini ukweli ni kwamba pengo lake lipo na haliwezi kuzibika kirahisi ndani ya Yanga, baadhi hawawezi kukubaliana na hili kutokana na hasira
Uwezekano wa kiungo huyo kurejea kuendelea na majukumu Jangwani ni mkubwa kutokana na jitihada zinazoendelea kufanywa kwani endapo Feisal atakaidi huenda akakutana na adhabu ya kufungiwa kucheza soka kwa muda mrefu.